Na mwandishi wetu Rais wa Marekani, Donald Trump, ameondolewa ghafla jukwaani baada ya kusikika milio ya risasi iliyovuruga hafla ya White House Correspondents' Dinner iliyokuwa ikiendelea jijini Washington, D.C. usiku wa kuamkia leo, Jumapili Aprili 26, 2026.Kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka vyombo vya usalama, tukio hilo lilitokea baada ya mshukiwa mwenye silaha kujaribu kuvamia eneo la ukaguzi lililokuwa chini ya ulinzi mkali wa maofisa wa usalama. Katika purukushani hizo, risasi zilifyatuliwa na kusababisha taharuki kubwa miongoni mwa wageni, wakiwemo waandishi wa habari na viongozi wa serikali waliohudhuria hafla hiyo.
Muda mfupi kabla ya tukio, Trump alikuwa akihutubia jukwaani. Aliondolewa haraka na walinzi wake pamoja na mkewe, Melania Trump, huku maofisa wengine waandamizi wa serikali, akiwemo wajumbe wa baraza la mawaziri, wakipelekwa maeneo salama.Katika ujumbe wa awali baada ya tukio, Trump alinukuliwa akisema, “Urais ni kazi yenye hatari, lakini hatuwezi kuishi kwa hofu.”
Mshukiwa wa tukio hilo, mwenye umri wa miaka 31 kutoka jimbo la California, amekamatwa na anashikiliwa na vyombo vya dola huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo na dhamira ya shambulio hilo. Tukio hili limeibua upya mjadala kuhusu usalama wa viongozi wa umma pamoja na ongezeko la matukio ya vurugu za kutumia silaha nchini Marekani. Mwisho.
0 Comments