Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

WIVU WA MAPENZI WAUA MUUGUZI (25) KINYAMA SAME—ALIYEMLIPIA ADA AIBUKA KUHUSISHWA.

 

Asha Abdallah Bakari(25) enzi za uhai wake.

Alisaidiwa Kusomeshwa na Mtuhumiwa, Mapenzi Mapya Yadaiwa Kuchochea Mauaji
Na marykitoto 
Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imekumbwa na tukio la kusikitisha baada ya muuguzi wa Hospitali ya Mji Same, Asha Bakari (25), kudaiwa kuuawa kikatili kwa kuchomwa kisu shingoni na mtu anayetajwa kuwa mpenzi wake.
Akithibitisha tukio hilo Aprili 21, 2026, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kaslida Mgeni, alisema mauaji hayo yalitokea Aprili 20, 2026 katika Kata ya Kisima, karibu na hospitali ambayo marehemu alikuwa akifanya kazi kwa kujitolea.
Kwa mujibu wa mkuu huyo, tukio hilo lilitokea majira ya saa tatu usiku nyumbani kwa marehemu, baada ya mtuhumiwa kudaiwa kumpigia simu akimtaka wakutane.
“Inadaiwa alipofika nyumbani kwake ndipo aliposhambuliwa na kuchomwa kisu shingoni,” alisema Mgeni, akirejea taarifa za Jeshi la Polisi.
Mgeni aliongeza kuwa muuguzi huyo alifariki dunia muda mfupi baada ya tukio hilo kutokana na majeraha aliyoyapata.
CHANZO CHA MAUAJI CHAFICHUKA
Kwa mujibu wa taarifa za awali, marehemu alidaiwa kuwa na uhusiano na wanaume wawili, ambapo mmoja wao ndiye aliyemsaidia kumsomesha hadi kufikia kupata ajira.
Hata hivyo, baada ya kuanza kazi hospitalini hapo, alidaiwa kuanzisha uhusiano mwingine na mfanyakazi mwenzake—hali iliyodaiwa kumkera mtuhumiwa na kusababisha mgogoro uliomalizika kwa mauaji.
MTUHUMIWA ATOROKA
Mgeni alisema mtuhumiwa, anayetajwa kuwa dereva wa bodaboda, alitoroka mara baada ya tukio na juhudi za kumkamata zinaendelea.
“Tayari tumemtambua kwa jina na kazi yake, na tunaendelea kumsaka,” alisisitiza.
DIWANI AZUNGUMZA
Akitoa maoni yake, Diwani wa Kata ya Kisima, Kei Mbwambo, alisema tukio hilo ni la kinyama na limeacha simanzi kubwa kwa wakazi.
“Ni pigo kubwa kwa jamii. Marehemu alikuwa bado kijana na ndiyo kwanza ameanza kuwahudumia wananchi,” alisema.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi huku likiwataka wananchi kutoa ushirikiano ili mtuhumiwa akamatwe.
Mwisho 

Post a Comment

0 Comments