Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akijibu swali Bungeni
Na marykitoto
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema serikali imejipanga kutekeleza ujenzi wa kilometa 50 za barabara ya lami katika kipande cha Bariadi–Sibiti hadi Singida, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha miundombinu ya usafiri nchini.
Akijibu swali Bungeni, Kasekenya alieleza kuwa tayari kuna mkandarasi anayesubiri kulipwa malipo ya awali ili kuanza kazi hiyo, ambayo pia itahusisha ujenzi wa daraja la Mto Sibiti kwa pande zote za Singida na Simiyu.
Swali hilo liliulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Simiyu, Tina Chenge, aliyetaka kufahamu ni lini serikali itaanza ujenzi wa barabara ya lami inayounganisha Bariadi, Lagangabili, Mwanhuzi, Sibiti, Iguguno hadi Singida, kwa kuzingatia sera ya kuunganisha makao makuu ya mikoa kwa barabara za lami.
Katika majibu yake, Kasekenya alimhakikishia mbunge huyo kuwa maandalizi yanaendelea, na utekelezaji wa mradi huo utaanza mara baada ya taratibu muhimu kukamilika.
Mradi huo unatarajiwa kuboresha mawasiliano na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mikoa ya Simiyu na Singida.
Mwisho.



0 Comments