Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA: MIMI NI YULE YULE — ASISITIZA FALSAFA YA MARIDHIANO NA KULINDA AMANI NCHINI.

 


Na mwandishi wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa hajabadilika kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidai kwenye mitandao ya kijamii, akieleza kuwa bado anaendelea kushikilia misingi ile ile ya uongozi wake tangu alipoingia madarakani.

Akizungumza leo Alhamisi, Aprili 23, 2026, Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema kuwa yeye ni yule yule anayeamini katika falsafa ya maridhiano (4R), na kwamba anachohitaji ni ushirikiano wa Watanzania ili kufanikisha dira hiyo.

“Wakati nafuatilia uwasilishaji wa ripoti hii nilisikia sentensi inayosema ‘Tunamtaka Samia wetu tunayemfahamu’ – kana kwamba nilipoingia nilikuwa Samia mwingine na sasa ni Samia mwingine. Nataka niwahakikishie Watanzania kuwa mimi ni Samia yuleyule wa falsafa ya maridhiano (4R). Ninachotaka ni ushirikiano wenu katika kutekeleza falsafa hiyo,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amewasihi Watanzania kutokubali kurubuniwa au kuchochewa na baadhi ya wanaharakati, wanasiasa na watu wenye maslahi binafsi wanaoweza kuhatarisha tunu ya amani ya nchi.

Amesisitiza kuwa mshikamano na ushirikiano wa pamoja ni muhimu katika kuijenga Tanzania yenye umoja, amani na maendeleo endelevu.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments