Majeneza yakiwa dukani. Picha na Mtandao
Na mwandishi wetu
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure imemsimamisha kazi mmoja wa watumishi wake wa kitengo cha mochwari kufuatia tuhuma za kuwashinikiza wafiwa kununua majeneza kutoka kwake binafsi.
Taarifa hiyo imetolewa na Ofisa Habari wa hospitali hiyo, Elidaima Kimaro, siku ya Jumatano, Aprili 22, 2026. Amesema kuwa mtumishi huyo anadaiwa kujihusisha na biashara ya majeneza kinyume na maadili ya utumishi wa umma, huku akiwalazimisha wafiwa kununua bidhaa hizo kutoka kwake.
“Tumepokea taarifa kuhusu mtumishi wa kitengo cha mochwari anayeuza majeneza na kulazimisha wafiwa kununua kwake. Uongozi wa hospitali umechukua hatua za haraka kwa kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi wa kina wa tuhuma hizo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Uongozi wa hospitali umeeleza kuwa hautavumilia vitendo vinavyokiuka maadili ya kazi na vinavyoweza kuwaongezea mzigo wafiwa katika kipindi kigumu cha maombolezo.
Uchunguzi unaendelea, na hatua zaidi zitachukuliwa kulingana na matokeo yatakayopatikana.Mwisho.
0 Comments