Na marykitoto
Mrajis wa Vyama vya Ushirika nchini, Dkt. Benson Ndiege, amevitaka Vyama vya Ushirika vya Mazao kuhakikisha vinatumia mizani za kidijitali katika upimaji wa mazao ya wakulima, hatua inayolenga kuondoa udanganyifu na kulinda maslahi ya wakulima.
Maelekezo hayo yametolewa kupitia barua ya tarehe 13 Machi, 2026, aliyowaandikia wenyeviti pamoja na wajumbe wa bodi wa vyama hivyo Tanzania Bara. Katika barua hiyo, Dkt. Ndiege alisisitiza umuhimu wa matumizi ya mizani za kidijitali ili kuhakikisha upimaji sahihi wa mazao na kurahisisha upatikanaji wa takwimu za uhakika kuhusu makusanyo na mauzo.
Aidha, alionya kuwa vyama vitakavyobainika kuwa na mizani hiyo lakini havitumii au vinaitumia kinyume na malengo yaliyokusudiwa, vitachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wa wakulima, wamehimizwa kuhakikisha mazao yao yanapimwa kwa kutumia mizani iliyounganishwa na Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU), ili waweze kupata malipo sahihi kulingana na uzito halisi wa mazao yao.
Vilevile, vyama vyote ambavyo bado havijanunua mizani za kidijitali vimetakiwa kukamilisha ununuzi huo ifikapo Juni 31, 2026, kwa kuzingatia taratibu za manunuzi pamoja na mwongozo uliotolewa na Ofisi ya Mrajis.
Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Tume ya Maendeleo ya Ushirika kuimarisha usimamizi wa vyama vya ushirika nchini, ambapo kipaumbele kwa sasa ni kuhakikisha uwepo na matumizi sahihi ya mizani za kidijitali katika sekta ya mazao.
#Toa maoni yako namna lumbesa inavyowanyonya wakulima

0 Comments