Na marykitoto
INSPECTOR MWINJUMA OMARY _MKAGUZI KATA YA SOMANDA (MJI WA SERIKALI )
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Mji wa Serikali (Somanda), wananchi wanahimizwa kuchukua tahadhari madhubuti ili kuepuka ajali na madhara yanayoweza kuzuilika. Usalama wa jamii unategemea hatua za kila mmoja wetu.
Kwanza, kwa yeyote mwenye kisima au shimo la aina yoyote, ni muhimu kuhakikisha kuwa limefunikwa vizuri au limezungushiwa uzio, hata kama ni wa muda kama wa mibao au miiba. Hatua hii itasaidia kuzuia ajali, hasa kwa watoto na wanyama.
Pili, wafugaji wanashauriwa kutowaacha watoto kwenda kuchunga peke yao. Imeonekana mara kadhaa watoto wakichezea maji, kujaribu kuvua samaki au hata kuogelea katika maeneo hatarishi, jambo linaloweza kusababisha kuzama na kupoteza maisha.
Aidha, wazazi na walezi wote wanapaswa kuendelea kuwa makini kwa kuhakikisha watoto hawachezi kwenye maji, iwe ni yanayotiririka au yaliyotuama, kwani yote yanaweza kuwa hatari.
Katika hali yoyote ya dharura au tukio lisilo la kawaida, usisite kutoa taarifa haraka kwa Mkaguzi wa Kata (Polisi Kata) au viongozi wa Serikali za Mitaa, wakiwemo Mtendaji na Mwenyekiti wa eneo husika, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.
Kumbuka: Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuchukua tahadhari dhidi ya athari za mvua katika maeneo yetu.
Polisi Jamii – kwa usalama na maendeleo ya wote.
🙏🏻🙏🏻🙏🏻🙏🏻🙏🏻🙏🏻🙏🏻🙏🏻

0 Comments