Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi.Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 40, mkazi wa Kijiji cha Songambele wilayani Shinyanga, amepoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha baada ya kukutwa akiwa na majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea katika Kitongoji cha Machongo, ambapo mwili wa marehemu ulipatikana nyumbani kwake, hali iliyoibua hofu na maswali mengi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Razaro Enock, alisema kuwa mazingira ya kifo hicho yana utata mkubwa.
“Mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha, na kulikuwa na migogoro ya kifamilia kabla ya tukio. Hata hivyo, chanzo halisi bado kinachunguzwa,” alisema Enock.
Taarifa zinaeleza kuwa marehemu alikuwa na mgogoro na mume wake, huku pia akidaiwa kuwa na uhusiano na mwanaume mwingine aliyekuwa akiishi naye kwa muda akijitambulisha kama ndugu, jambo lililokuja kubainika kuwa si kweli.
Inadaiwa kuwa baada ya kutofautiana, mwanaume huyo aliondoka na baadhi ya mali zake, na muda mfupi baadaye ndipo tukio hilo la kifo lilipotokea, hali inayozua maswali zaidi juu ya mazingira halisi ya tukio hilo.
Watoto wa marehemu nao wanadaiwa kueleza kuwa siku ya tukio, mwanaume huyo alifika usiku na kuwahimiza walale mapema, jambo linaloongeza hisia za uwezekano wa kuhusika kwake.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi wa awali unaonesha dalili za matumizi ya nguvu.
“Inaonekana marehemu alipigwa kwa kitu kigumu sehemu mbalimbali za mwili wake, ikiwemo kichwani. Tunamshuku mume wake ambaye alitoroka baada ya tukio,” alisema SACP Magomi.
Ameongeza kuwa chanzo kinachodhaniwa ni wivu wa mapenzi, huku juhudi za kumtafuta mtuhumiwa huyo zikiendelea ili achukuliwe hatua za kisheria.
Jeshi la Polisi limelaani tukio hilo na kutoa wito kwa jamii kuepuka migogoro ya vurugu, badala yake kutumia njia za amani kutatua tofauti zao.
Uchunguzi wa kina bado unaendelea, huku wananchi wakihimizwa kushirikiana na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa mtuhumiwa.
#Unamaoni gani juu matendo haya ya kikatili katika familia?
0 Comments