Na marykitoto

Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limemkamata kijana Ibrahimu Mugendi kwa tuhuma za kukusanya michango isivyo halali baada ya kujifanya bubu akidai anahitaji msaada wa matibabu.
Mtuhumiwa huyo, ambaye ni mkazi wa Mkoa wa Kigoma, anadaiwa kutumia mbinu ya kujifanya hawezi kuongea ili kuomba michango kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Hata hivyo, njama zake zilifichuliwa na kusababisha kukamatwa kwake na vyombo vya dola.
Akizungumza na KITOTO DIGITAL leo, Machi 27, 2026, Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Issa Suleiman, alisema Mugendi aliwasili mkoani humo Februari 18, 2026 na kufikia katika moja ya nyumba za kulala wageni.
Kwa mujibu wa Kamanda Suleiman, Februari 26, 2026 mtuhumiwa alifika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara kuomba kibali cha kuchangisha fedha, akieleza kuwa anasumbuliwa na tatizo la kiafya linalomfanya ashindwe kuongea.
Hata hivyo, uchunguzi wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa kijana huyo hakuwa na tatizo lolote la kuongea, bali alitumia udanganyifu huo kama njia ya kujipatia fedha kutoka kwa wananchi.
Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuwa makini wanapotoa misaada na kuhakikisha wanathibitisha uhalali wa waombaji ili kuepuka matukio ya udanganyifu kama hayo.
0 Comments