Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

MADAKTARI SITA WAJERUHIWA AJALI WAKIMKWEPA MPANDA BAISKELI

 Na marykitoto 






Madaktari sita kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou-Toure wamejeruhiwa kufuatia ajali ya gari waliyokuwa wakisafiria wakirejea kutoka kambi ya matibabu ya kibingwa Wilayani Kwimba.

Ajali hiyo ilitokea Machi 27, 2026 majira ya saa 12:30 jioni katika barabara ya Jojiro, kijiji cha Maremve, Kata ya Igongwa, Wilaya ya Kwimba.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, gari hilo lenye namba T.231 AWT aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop lilikuwa likiendeshwa na Dkt. James Nkya (38), mkazi wa Lumala-Pasiansi, Wilaya ya Ilemela.

Inaelezwa kuwa madaktari hao walikuwa wakirejea Mwanza mjini baada ya kutoa huduma za kibingwa katika Hospitali ya Icheja. Walipofika eneo la tukio, dereva alijaribu kumkwepa mpanda baiskeli aliyekuwa ameanguka katikati ya barabara ya vumbi.

Katika harakati za kukwepa, gari hilo lilipoteza mwelekeo, likaacha barabara, kugonga gema na hatimaye kupinduka, na kusababisha majeruhi kwa abiria waliokuwamo ndani.

Majeruhi hao ni pamoja na Dkt. James Nkya na Dkt. Self Mmka, ambao wamelazwa katika Hospitali ya Sekou-Toure. Wengine ni Dkt. Stanley Makundi na Dkt. Avetha Masawe waliolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando.

Madaktari wengine wawili, Dkt. Mary Urasa na Dkt. Frank Mgeta, walipata majeraha lakini tayari wametibiwa na kuruhusiwa baada ya hali zao kuimarika.

Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa majeruhi wanne bado wanaendelea na matibabu huku wawili wakiwa wameruhusiwa.

Kamanda Mutafungwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni juhudi za dereva kukwepa ajali kwa mpanda baiskeli aliyeanguka barabarani.

Ametoa wito kwa watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria na tahadhari za usalama ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments