
Sio mafuta tu, hadi kondomu.
Mvutano wa kivita unaoendelea umeanza kuacha alama si tu katika siasa za kimataifa, bali pia kwenye sekta za uzalishaji—ikiwemo bidhaa muhimu kama kondomu. Athari zake zinaanza kujitokeza wazi, huku wadau wa viwanda wakionya juu ya uwezekano wa kupanda kwa bei katika siku za karibuni.
Chanzo kikubwa cha hofu ni kuvurugika kwa upatikanaji wa malighafi muhimu kama amonia na mafuta ya silikoni, ambazo zote zinategemea bidhaa za petroli. Malighafi hizi zina mchango mkubwa katika utengenezaji wa kondomu—amonia ikitumika kuimarisha mpira na kuondoa protini zisizohitajika, huku mafuta ya silikoni yakitumika kama kilainishi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa wauzaji nchini India, kuna dalili kuwa bei ya amonia inaweza kupanda kwa asilimia 40 hadi 50. Ongezeko hilo linaweza kusababisha pia kupanda kwa gharama ya mafuta ya silikoni, na hatimaye kuathiri bei ya mwisho ya bidhaa sokoni.
Afisa mmoja wa sekta hiyo, aliyenukuliwa na BBC Hindi kwa sharti la kutotajwa jina, alikiri kushangazwa na hali hiyo akisema, “Hakuna aliyedhani kuwa kutakuwa na changamoto yoyote kwenye bidhaa kama kondomu.”
Ikiwa hali itaendelea hivi, watumiaji wa kawaida wanaweza kukumbana na ongezeko la bei madukani, jambo litakaloweza pia kuathiri upatikanaji na matumizi ya bidhaa hii muhimu ya afya ya uzazi.
Mwisho.
0 Comments