Tume ya uchunguzi imeongezewa muda kufuatia wingi wa ushahidi na mwitikio mkubwa wa wananchi.
Mamlaka ya Uteuzi imetoa nyongeza ya siku 21 kwa Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Kufuatia uamuzi huo, Tume sasa inatarajiwa kukamilisha kazi zake ifikapo Aprili 24, 2026.
Hatua hii inalenga kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa kina, umakini na ufanisi wa hali ya juu. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa, muda huo wa ziada utaiwezesha Tume kukamilisha uchambuzi wa ushahidi, taarifa pamoja na maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali.
Aidha, wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi wanatarajiwa kutumia muda huo kuchambua vielelezo vipya vilivyowasilishwa, hatua inayochangia upatikanaji wa matokeo sahihi na yenye kuaminika.
Sambamba na hilo, Tume itatumia muda huo kukamilisha maandalizi ya ripoti yake ya mwisho itakayowasilishwa kwa Rais, pamoja na kuandaa tafsiri ya ripoti hiyo kwa ufasaha.
Tume ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake tarehe Novemba 20, 2025, ikiwa na lengo la kukamilisha kazi ndani ya siku 90. Hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali, muda huo uliongezwa hadi Aprili 3, 2026—lakini haukutosha.
Katika kipindi hicho, mwitikio wa wananchi ulikuwa mkubwa kuliko ilivyotarajiwa, huku watu wengi wakijitokeza kutoa ushahidi, kutuma taarifa na maoni kupitia njia mbalimbali. Hali hii ilisababisha kuongezeka kwa kazi ya uchambuzi.
Kutokana na wingi huo wa taarifa, Tume haikuweza kukamilisha kazi ndani ya muda uliotolewa, hivyo kuwasilisha ombi la nyongeza ya muda ambalo sasa limekubaliwa rasmi.
Tume imeendelea kutoa shukrani za dhati kwa wananchi na wadau wote waliochangia katika zoezi hili, wakiwemo waliotoa ushahidi moja kwa moja, waliotuma taarifa kwa njia ya simu, ujumbe mfupi, maandishi pamoja na kupitia mitandao ya kijamii.
Mwisho.
0 Comments