Na marykitoto
Hali ya taharuki ilitanda katika Parokia ya Kagunguli, Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza, baada ya kijana mmoja anayesadikiwa kuwa na matatizo ya akili kuwashambulia waumini wawili kwa kutumia panga wakati wa ibada, kabla ya yeye mwenyewe kupoteza maisha kufuatia kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali.
Kwa mujibu wa taarifa, tukio hilo lilihusisha kijana aliyefahamika kwa jina la Renatus Silivester (38), maarufu kama “Pacome”, mkazi wa kijiji hicho. Inadaiwa kuwa aliingia kanisani kupitia mlango wa upande wa kulia akiwa amebeba mfuko na kuelekea moja kwa moja madhabahuni, jambo lililozua taharuki miongoni mwa waumini.
Mwenyekiti wa parokia hiyo, Costantine Muumba Bituro (65), alishtukia mienendo ya kijana huyo na kumtoa nje ya kanisa. Hata hivyo, wakati wakijaribu kumhoji, kijana huyo alitoa panga na kuwajeruhi waumini wawili kabla ya kudhibitiwa.
Baada ya tukio hilo, kundi la wananchi na waumini waliokuwa nje ya kanisa walimvamia mtuhumiwa na kumpiga kwa silaha za jadi, hali iliyosababisha kupata majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili wake.
Mtuhumiwa alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe kwa matibabu, lakini alifariki dunia njiani kabla ya kufikishwa hospitalini.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limethibitisha tukio hilo na linaendelea na uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha tukio hilo, huku likifuatilia pia hali za majeruhi waliolazwa hospitalini wakipatiwa matibabu.
Mwisho.
0 Comments