Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

POLISI YAONYA DHIDI YA UVUMI WA ‘SEHEMU ZA SIRI KUPOTEA.

 Na marykitoto 


Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa onyo kali kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaosambaza taarifa za uzushi zisizo na uthibitisho wa kisayansi kuhusu madai ya wanaume kupoteza sehemu zao za siri baada ya kuguswa mabegani. Uvumi huo, ulioripotiwa katika mikoa ya Songwe, Mbeya na Dar es Salaam, umeibua taharuki kubwa na kusababisha vifo vya watu watano pamoja na majeruhi kadhaa wanaoendelea kupatiwa matibabu.

Onyo hilo limetolewa leo Jumamosi, Aprili 4, 2026, kupitia taarifa rasmi iliyosainiwa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime. Polisi pia wametangaza kuanza uchunguzi wa kina pamoja na msako mkali dhidi ya walioanzisha na kueneza uvumi huo, huku wakichunguza nia halisi ya kusambaza taarifa hizo za kupotosha umma.


Akizungumza kwa msisitizo, DCP Misime ameeleza kuwa madai hayo hayana ukweli wowote na yanachochewa na imani za kishirikina, mihemko ya makundi na malengo yasiyojulikana. Amefafanua kuwa uchunguzi uliofanywa kwa wanaodai kuathirika umebaini kuwa hawakuwa na mabadiliko yoyote ya kimwili, huku wanaodai kushuhudia matukio hayo wakishindwa kutoa ushahidi au kumtambua mhusika yeyote.


Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, uvumi huo ulianza Tunduma, mkoani Songwe, Aprili 1, 2026, na kusababisha vifo pamoja na majeruhi. Baadaye, matukio kama hayo yaliripotiwa Makongolosi jijini Mbeya na kisha kuenea hadi maeneo ya Kimara Mwisho na Mbezi Shule jijini Dar es Salaam. Hadi leo, matukio mapya yameendelea kuripotiwa Mbeya, yakisababisha majeruhi zaidi, ingawa uchunguzi wa kitabibu umeendelea kuthibitisha kuwa madai hayo hayana msingi wowote.


Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuwa watulivu, kupuuza uvumi huo na kuepuka kuchukua sheria mkononi, huku likisisitiza kuwa yeyote atakayebainika kuhusika na uchochezi au usambazaji wa taarifa za uongo atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Mwisho .

Post a Comment

0 Comments