Kamanda wa jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi.
Na marykitoto
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi, amethibitisha kutokea kwa tukio la kusikitisha la kifo cha mwanafunzi mmoja wa kidato cha nne, Rebecka Boniphace Maganga (17), aliyekuwa akisoma katika Shule ya Sekondari Old Shinyanga.
Inadaiwa kuwa mwanafunzi huyo amefariki dunia baada ya kujinyonga ndani ya chumba alichokuwa akiishi, akitumia mkanda wa sketi ya shule. Tukio hilo limetokea Aprili 27, 2026 majira ya saa saba mchana katika eneo la Old Shinyanga.
Kwa mujibu wa Kamanda Magomi, jeshi la polisi lilipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa mlezi wa marehemu, Mashala Piter (56), ambaye ndiye aliyegundua kifo hicho. Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa tukio hilo linaweza kuwa limechangiwa na msongo wa mawazo.
Inaelezwa kuwa kabla ya tukio hilo, mwanafunzi huyo alirejeshwa nyumbani na walimu wake baada ya kutohudhuria masomo kwa muda wa wiki mbili bila taarifa, akitakiwa kurejea shuleni akiwa ameambatana na mzazi au mlezi wake.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Senyenge, Benjamin Andrew, amesema walipokea taarifa za tukio hilo majira ya saa sita mchana na walipofika eneo la tukio walimkuta tayari amefariki dunia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Manispaa ya Shinyanga, Bi. Meryester Nyalusanda, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuimarisha mawasiliano na watoto wao ili kubaini mapema changamoto wanazokabiliana nazo.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kwa ajili ya uchunguzi zaidi, huku jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Mwisho.
0 Comments