Akizungumza jijini Dar es Salaam katika mkutano wa kitaifa kuhusu viashiria vya ukatili wa kijinsia vinavyofanyika kupitia teknolojia (TFGBV), Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Abeda Rashid Abdallah, amesema kuwa tatizo hilo linaongezeka kwa kasi na linahitaji hatua za haraka. Mkutano huo umeandaliwa na Shirika la Kimataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) kwa kushirikiana na Shirika la C-Sema, ukiwa na lengo la kuimarisha juhudi za Tanzania katika kukabiliana na ongezeko la ukatili wa kidijitali dhidi ya wanawake na watoto.

Abeda alifafanua kuwa ukatili huo unajumuisha vitendo kama usambazaji wa picha za faragha bila ridhaa, unyanyasaji wa kingono mtandaoni, vitisho vya kidijitali, pamoja na lugha za chuki na matusi, vitendo vinavyoathiri ustawi wa kisaikolojia na kijamii wa waathirika, hususan wanawake na wasichana. Alibainisha kuwa zaidi ya nusu ya wanawake vijana wamekumbwa na unyanyasaji mtandaoni, hali inayozua wasiwasi mkubwa hasa wakati ambapo matumizi ya teknolojia yanaongezeka kwa kasi nchini. Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa UNFPA nchini Tanzania, Melissa Barrett,
alisisitiza kuwa teknolojia inapaswa kuwa chombo cha kuwawezesha watu badala ya kuwa jukwaa la kuumiza. “Ni muhimu ubunifu wa kidijitali uchangie katika kukuza usalama na usawa wa kijinsia,” alisema Barrett.
“Aidha, Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Zitting, alisema kupitia ushirikiano kati ya serikali ya Finland, UNFPA, na Serikali ya Tanzania, wanashirikiana kuboresha usalama wa mtandao, utawala wa kidijitali na matumizi ya teknolojia yenye maadili. Juhudi hizo zinalenga kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanasaidia kupunguza ukatili wa kijinsia badala ya kuongeza pengo.
Mwisho.
0 Comments