Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

SIMIYU YATIKISA DODOMA: NJALU SILANGA AONGOZA WABUNGE KWENYE MKUTANO MKUBWA WA MAGEUZI YA PAMBA.

 

      


 Na marykitoto.

MBUNGE wa Jimbo la Itilima Mkoani Simiyu, Njalu Silanga, ameongoza Wabunge wa Mkoa huo kushiriki Mkutano mkubwa wa Wadau wa Pamba uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre (JKC) jijini Dodoma, ukilenga kujadili na kuboresha sekta ya pamba nchini. 

Mkutano huo umefunguliwa na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, ambaye amesisitiza kuwa Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inaendelea kushirikiana bega kwa bega na wadau wa sekta ya kilimo ili kuboresha huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa.

           


Chongolo ameeleza kuwa tasnia ya pamba imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za ugani kupitia Bodi ya Pamba Tanzania, kwa kushirikiana na kampuni binafsi zinazohudumia wakulima moja kwa moja mashambani.

Akitoa mchango wake, Mbunge Njalu Silanga ameitaka serikali kupitia Wizara ya Kilimo kushirikiana kwa karibu zaidi na wataalamu wa kilimo ili kuhakikisha uzalishaji wa pamba unaanzia ngazi ya chini kwa ufanisi mkubwa. Amesisitiza kuwa utaalamu ni nguzo muhimu isiyoweza kupuuzwa katika kuongeza tija.

        



Aidha, Njalu amewapongeza wakulima wanaozalisha pamba kwa tija, akibainisha kuwa motisha zinazotolewa na serikali, ikiwemo zawadi kwa wakulima bora, zimeongeza ari na ushindani chanya katika uzalishaji.

       

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba, Marco Mtunga, amesema kuwa zao la pamba lina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa na limekuwa chanzo kikuu cha ajira kupitia mnyororo mzima wa thamani.

Mtunga amefafanua kuwa serikali imeboresha huduma za ugani kupitia programu ya BBT, ambapo mwaka 2023/24 walianza na kata 40, wakaongezeka hadi kata 232 mwaka 2024/25, na kufikia kata 589 mwaka 2025/26 — hatua inayoonesha ukuaji mkubwa wa huduma hizo.

Mkutano huo umehudhuriwa na Wabunge mbalimbali wa Mkoa wa Simiyu, wakiwemo Njalu Silanga (Itilima), Salum Khamis-Jambo (Meatu), Masanja Kadogosa (Bariadi Vijijini), Musa Mbuga (Meatu), Mashimba Ndaki (Maswa Mashariki), pamoja na Tinah Chenge na Ester Midimu (Viti Maalum). Wengine ni pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali kutoka mikoa 17 inayolima pamba, wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Maafisa Kilimo, wazalishaji, wanunuzi, na wadau wengine wa sekta hiyo.



Kwa ujumla, mkutano huo umeweka msingi imara wa mageuzi mapya katika sekta ya pamba, ukilenga kuongeza tija, ajira na mchango wa zao hilo katika uchumi wa taifa.

Mwisho. 





Post a Comment

0 Comments