Na OWM - TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (OWM-TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe ameelekeza hatua za haraka zichukuliwe kuwarejesha wafanyabiashara wa Soko la Mawasiliano (Simu 2000) kuendelea na shughuli zao, baada ya soko hilo kupigwa na ajali ya moto Aprili 4, 2026.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri Shemdoe alipofika kutembelea soko hilo Aprili 10, 2026, na kuridhishwa na utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba aliyoyatoa Aprili 6, 2026, alipokagua madhara ya tukio hilo na kuelekeza soko kusafishwa mara moja.
"Nimeridhishwa na utekelezaji wa maelekezo aliyotupatia Rais na Waziri Mkuu, hivyo naelekeza haraka iwezekanavyo wafanyabiashara warejeshwe kuendelea na shughuli zao lakini wasijenge vibanda na badala yake waweke meza pamoja na miamvuli ili kujikinga dhidi ya jua na mvua," amesisitiza Shemdoe.
Waziri Shemdoe amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila kusimamia kikamilifu maelekezo hayo, huku akimtaka Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando kufanya ufuatiliaji wa kila siku ili wafanyabiashara warejee haraka.
Mkuu wa Mkoa, Chalamila amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando kwa usimamizi mzuri wa utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu, ambayo yamewezesha urejeshwaji wa haraka wa wafanyabiashara walioathirika.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amesema ameelekeza zoezi la utambuzi wa wafanyabiashara wote lifanyike ndani ya siku tatu, wakiwasilisha majina matatu na vitambulisho, ili kuepuka tatizo la watu kuchukua vibanda na kuwapangishia wengine. Aidha, amehakikisha kwamba mikopo itatolewa kwa wafanyabiashara waliothirika tu na wenye sifa stahiki.
0 Comments