Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

RPC MUTAFUNGWA ATOA WITO WA UTULIVU UKEREWE, AONYA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI.

 


Na Dawati la Habari Polisi Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewataka wakazi wa Wilaya ya Ukerewe kuwa watulivu kufuatia tukio lililosababisha taharuki baada ya kijana mmoja, Leonard Mganga (44), kuvamia kanisa na kuwajeruhi waumini wawili kabla ya kupoteza maisha.

Tukio hilo lilitokea Aprili 5, 2026, majira ya saa 1:30 asubuhi katika Kanisa la Bikira Maria Mama wa Tumaini Jema, Parokia ya Kagunguli, Jimbo Katoliki la Bunda, wakati wa Misa Takatifu ya Dominika ya Pasaka.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa aliingia kanisani kupitia mlango wa pembeni akiwa amebeba mfuko uliokuwa na panga, kisha kuwashambulia waumini wawili baada ya kutolewa nje, hali iliyosababisha taharuki kubwa kanisani hapo. Baadaye, mtuhumiwa huyo alishambuliwa na waumini pamoja na wananchi waliokuwepo eneo la tukio na hatimaye kufariki kutokana na majeraha.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Kagunguli, viongozi wa dini na watumishi wa serikali Aprili 10, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbroad Mutafungwa, amesema kumekuwepo na matukio yanayoleta hofu na taharuki kwa wananchi wa Ukerewe na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla.



Ametaja matukio mengine kuwa ni pamoja na madai ya uwepo wa watu wanaojiita “Kamchape” wanaodai kuondoa uchawi na kuwahadaa wananchi, tukio la binti wa miaka 18 wa kidato cha tatu aliyeripotiwa kupotea na kuonekana baadaye akiwa hai, pamoja na tukio la uvamizi wa kanisa.



“Haya yote yameshughulikiwa kwa mujibu wa sheria. Tunawahimiza wananchi kutoa taarifa na kushirikiana na vyombo vya usalama badala ya kujichukulia sheria mkononi,” alisema Kamanda Mutafungwa.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu ya usalama na Polisi Jamii, huku akiagiza viongozi wa polisi wa wilaya na kata kuimarisha uhamasishaji wa jamii kuhusu amani na usalama.

Kwa upande wake, baadhi ya wakazi wa Kagunguli wameunga mkono elimu hiyo wakisema itasaidia kupunguza matukio ya uvunjifu wa amani na kuongeza ushirikiano kati ya wananchi na polisi.



Kamanda Mutafungwa pia ametembelea eneo la kanisa lilipotokea tukio pamoja na familia ya marehemu kupata taarifa zaidi za tukio hilo.



Mwisho.


Post a Comment

0 Comments