Kamanda wa polisi mkoani Arusha , Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo.
Na mwandishi wetu.
Jamii ya wakazi wa Sinoni jijini Arusha imekumbwa na simanzi na mshangao kufuatia tukio la kinyama lililotokea Aprili 28 majira ya jioni, ambapo mwanaume mmoja anadaiwa kumuua kikatili mtoto wake mchanga wa miezi nane.
Mtuhumiwa, Salmin Rajab (29), ambaye ni fundi ujenzi na mkazi wa eneo hilo, kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za mauaji ya mwanawe, Sahiri Salmin. Inadaiwa kuwa alitenda kitendo hicho cha kutisha kwa kumchinja mtoto shingoni na kutenganisha kichwa na kiwiliwili.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, SACP Justine Masejo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea.
“Tunamshikilia mtuhumiwa kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake wa miezi minane. Upelelezi ukiwa umekamilika, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” alisema.
Kwa mujibu wa jirani mmoja, Mirium Kivuyo, tukio hilo lilitokea wakati mke wa mtuhumiwa alipokuwa ametoka kwenda dukani kununua tambi, akiwa ameondoka na mtoto wao mwingine. Aliporudi nyumbani, alikuta mlango umefungwa kwa ndani. Baada ya kugonga, mume wake alifungua mlango akiwa katika hali ya sintofahamu, akapiga magoti na kuanza kuomba msamaha huku akidai kuwa tayari amemuua mtoto.
Tukio hilo limeacha maswali mengi bila majibu miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku wengi wakishindwa kuelewa chanzo cha ukatili huo dhidi ya mtoto asiye na hatia.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini sababu na mazingira halisi ya tukio hilo, huku jamii ikihimizwa kutoa ushirikiano kwa mamlaka na pia kuwa makini na viashiria vya matatizo ya kisaikolojia au migogoro ya kifamilia ambayo inaweza kusababisha matukio ya aina hii.
Hili ni tukio la kusikitisha linalotukumbusha umuhimu wa afya ya akili, mawasiliano katika familia, na ulinzi wa watoto wadogo ambao hawawezi kujitetea.
Mwisho.
0 Comments