Na marykitoto

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi SACP Marco Chilya akiwa ameshika sare za Jeshi ambazo mtuhumiwa huyo alikua akizitumia wakati wa kutenda uhalifu wake
Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limefanikiwa kufichua mbinu mpya na ya kutisha inayotumiwa na baadhi ya wahalifu kujipenyeza katika jamii—kujifanya askari kwa kutumia sare za vyombo vya ulinzi na usalama.
Katika operesheni maalum iliyofanyika Machi 31, 2026, polisi walimkamata Michael Ngonyani (38), mkazi wa Mtyangimbole, anayehusishwa na mtandao wa wizi wa magari unaodaiwa kuenea katika mikoa mbalimbali, ikiwemo .
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco G. Chilya, alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ni matokeo ya ufuatiliaji wa kina dhidi ya wahalifu wanaotumia mbinu zisizo za kawaida kujificha.
Mtuhumiwa alinaswa katika eneo la Mtyangimbole, Halmashauri ya Madaba, baada ya polisi kumfuatilia kwa muda.
Baada ya upekuzi kufanyika nyumbani kwake, polisi walikuta Gari aina ya Toyota IST lenye namba T.829 DYH ,Leseni nne za udereva, zote zikiwa na majina tofauti.
Ugunduzi huu umezua maswali mengi kuhusu utambulisho halisi wa mtuhumiwa na shughuli zake.
Katika upekuzi huo huo, vitu mbalimbali vinavyodhaniwa kuwa vya wizi vilipatikana, vikiwemo, Televisheni mbili (inchi 65 na 55) ,Sound bar aina ya Skywood na Mashine ya kusukuma maji (water pump) Polisi wanaendelea kuchunguza mali hizo ili kubaini wamiliki wake halali.
Katika tukio lililozua mshangao mkubwa, mtuhumiwa huyo alikutwa pia akiwa na Sare za Jeshi la Polisi (kaki) pamoja na Sare za JWTZ (suruali na fulana)
Inaelezwa kuwa alitumia sare hizo kujifanya askari ili kurahisisha utekelezaji wa uhalifu wake bila kutiliwa shaka.
Kamanda Chilya amesisitiza kuwa uchunguzi bado unaendelea, hususan kubaini ,Alikopata sare hizo Mtandao mzima anaoshirikiana nao.
Ameonya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na mtu yeyote atakayebainika kuhusika.
Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuwa makini na watu wanaojitambulisha kama askari bila uthibitisho rasmi, na kutoa taarifa mara moja wanapobaini viashiria vya uhalifu.
Mwisho.



0 Comments