Na marykitoto 
Wananchi wametakiwa kutopaniki na kununua mafuta kwa wingi, bali waendelee na ununuzi wa kawaida kwani nchi ina akiba ya kutosha ya mafuta na serikali tayari imechukua tahadhari kuhakikisha upatikanaji wake unaendelea kuwa wa uhakika.
Akizungumza Machi 25,2026 Jijini Dar es salaa wakati wa ziara ya kukagua hali ya upatikanaji wa mafuta katika maghala (depo), Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, James Mataragio, amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea hali halisi ya akiba ya mafuta pamoja na ufanisi wa usambazaji wake kutoka maghalani hadi kwa walaji.
Amesema serikali imepokea malalamiko kuhusu ucheleweshaji wa upakiaji wa mafuta kwenye malori pamoja na baadhi ya vituo kudai kukosa huduma hiyo, hivyo imeona ni muhimu kufuatilia kwa karibu ili kubaini ukweli na kuchukua hatua stahiki.
“Tunataka kuhakikisha mafuta yapo ya kutosha lakini pia yanatoka kwa wakati. Haiwezekani malori yapakiwe halafu yachelewe kuondoka bila sababu za msingi,” amesema.
Aidha, amekanusha madai kuwa ucheleweshaji unasababishwa na taratibu za kodi akieleza kuwa mamlaka husika zipo kwenye ziara hiyo kuthibitisha hali halisi na kuondoa visingizio visivyo na msingi.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amewapongeza waendeshaji wa maghala kwa kufanya kazi kwa bidii, ikiwemo kufanya kazi usiku na siku za mwisho wa wiki ili kuhakikisha huduma inaendelea kutolewa bila kukwama.
Hata hivyo, ameonya wafanyabiashara wanaojaribu kuficha mafuta ili kuyauza kwa bei ya juu baadaye, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, James Andilile, amesema licha ya changamoto za kimataifa zinazoathiri soko la mafuta, bado nchi ina akiba ya kutosha kukidhi mahitaji ya sasa.
Ameeleza kuwa ongezeko la gharama za uagizaji mafuta duniani, hususan kutoka Mashariki ya Kati, linaweza kuathiri bei, lakini serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha bei zinabaki himilivu.
Naye mwakilishi wa kampuni ya Camel Oil Tanzania, amesema kampuni hiyo ina akiba ya kutosha ya mafuta kwa miezi miwili hadi mitatu ijayo na imeendelea kusambaza mafuta kwa kiwango kinachokidhi mahitaji.
Nao, wadau wa sekta ya mafuta wamewahakikishia wananchi kuwa hakuna uhaba wa mafuta nchini, wakisisitiza kuwa hofu isiyo na msingi inaweza kusababisha upungufu wa bandia endapo wananchi watanunua mafuta kupita kiasi.

0 Comments