Na marykitoto
👉 🚨Je , wewe ni miongoni mwa wanaopenda kunywa chai ya moto inayounguza koo? Basi sikiliza hili kwa makini…
Daktari Bingwa wa Saratani kutoka Hospitali ya Ocean Road, Dk. Sadiq Siu, ametoa tahadhari kali kwa wananchi kuwa unywaji wa vinywaji vya moto kupita kiasi unaweza kuongeza hatari ya kupata saratani ya koo.
Akizungumza kuhusu ugonjwa huo, Dk. Sadiq amesisitiza kuwa ni muhimu kwa kila mmoja kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, kwani saratani inapogundulika mapema, huwa rahisi kutibika.
👉 “Watu wengi hupenda chai au uji wa moto sana hadi unaunguza koo—hii si tabia salama,” anasisitiza.
Kwa mujibu wa daktari huyo, joto kali linaweza kuathiri seli za ndani ya koo na kuzifanya zibadilike kitabia. Mabadiliko hayo husababisha seli kukua kwa kasi isiyo ya kawaida, hali inayoweza kupelekea kutokea kwa uvimbe—hatimaye kusababisha saratani.
Mbali na vinywaji vya moto kupita kiasi, sababu nyingine zinazochangia saratani ya koo ni pamoja na:
Uvutaji sigara
Matumizi ya ugoro
Unywaji pombe
Unene uliopitiliza
Dalili mojawapo muhimu ya ugonjwa huu ni ugumu wa kumeza chakula, hali inayotokea kutokana na uvimbe kupunguza njia ya chakula kupita.
Dk. Sadiq anaeleza kuwa saratani ya koo huwapata zaidi watu wenye umri wa miaka 40 na kuendelea, huku maeneo ya Kaskazini na Kaskazini Mashariki mwa Tanzania—ikiwemo Tanga, Kilimanjaro na Dar es Salaam—yakitajwa kuwa na ongezeko la visa vya ugonjwa huo.
Hata hivyo, kuna matumaini…
Matibabu ya saratani ya koo yanapatikana kupitia: ✔️ Upasuaji
✔️ Tiba ya kemikali (chemotherapy)
✔️ Tiba ya mionzi (radiotherapy)
📌 Ujumbe muhimu: Epuka kunywa vinywaji vya moto kupita kiasi na hakikisha unafanya uchunguzi wa afya mara kwa mara. Afya yako ni mtaji wako!
Mwisho.
Nini maoni yako kwa wale tulio zoea Chai moto, uji na gahawa inapo pungua moto tunaomba kuchemshiwa ??😆 😂
0 Comments