Na marykitoto
Mkoa wa Simiyu umeungana na dunia kuadhimisha Siku ya Wazimamoto Duniani leo tarehe 4Mei 2026 katika hafla iliyofanyika Wilaya ya Bariadi, katika Kiwanja cha Sabasaba (CCM), ambapo wananchi, wanafunzi na makundi mbalimbali ya kijamii wamejitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho hayo muhimu.
Tukio hilo limefanyika rasmi leo likilenga kuelimisha jamii kuhusu masuala ya usalama wa moto, uokoaji na namna bora ya kuzuia majanga ya moto kabla hayajatokea.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mrakibu Msaidizi wa Zimamoto, Faustin Mtitu ambaye pia ni Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Simiyu, amewakaribisha wananchi wote kushiriki kwa wingi, akisisitiza umuhimu wa elimu ya kujikinga na majanga ya moto.
“Tunawahimiza wananchi, hususan vijana na wanafunzi, kutumia fursa hii kupata elimu ya moja kwa moja kuhusu namna ya kujilinda na moto pamoja na kushirikiana na Jeshi la Zimamoto katika kuokoa maisha na mali,” amesema Mtitu.
Mbali na elimu hiyo muhimu, maadhimisho hayo yameambatana na matukio mbalimbali ya maonyesho ya vitendo vya wazimamoto, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya uokoaji, namna ya kutumia vifaa vya kuzimia moto, pamoja na elimu ya tahadhari za awali za majanga ya moto.
Pia kumefanyika michezo mbalimbali ya burudani, ikiwemo mechi ya mpira wa miguu kati ya timu ya Raha Queens na kidinda girls matokeo raha 2-0 michezo ambayo imevutia mashabiki wengi na kuongeza hamasa ya maadhimisho hayo. Michezo hiyo imelenga kuimarisha mshikamano kati ya Jeshi la Zimamoto na jamii pamoja na kutoa burudani kwa washiriki.
Wananchi waliohudhuria wameonekana kufurahia mafunzo na burudani hizo, huku wakipata nafasi ya kuuliza maswali na kujifunza kwa vitendo jinsi ya kukabiliana na majanga ya moto pindi yanapotokea.
Siku ya Wazimamoto Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 4 Mei duniani kote, ikiwa ni siku maalum ya kutambua mchango wa wazimamoto katika kuokoa maisha ya watu na mali, pamoja na kuhimiza jamii kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto.
Maadhimisho ya mwaka huu katika Simiyu yameweka msisitizo mkubwa katika elimu, ushirikiano na uhamasishaji wa jamii kuwa sehemu ya mfumo wa ulinzi dhidi ya majanga ya moto.
Mwisho.
0 Comments