Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

DC BARIADI AONYA VIKALI WANAOZUIA CHANJO YA POLIO KWA WATOTO.

 


Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu mhe.simon Simalenga (katika) akizungumza kwenye Kikao cha kuhamasisha chanjo ya polio. 

Na marykitoto 

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Simon Simalenga, amelionya Kanisa la Last Church of God kwa kuzuia watoto chini ya umri wa miaka 10 kupata chanjo ya polio, akisisitiza kuwa kitendo hicho ni kinyume cha sheria na kinahatarisha maisha ya watoto wakati serikali ikiendelea na kampeni ya awamu ya pili katika mikoa kadhaa ikiwemo Simiyu, Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga na Singida.


Akizungumza kwenye kikao cha kuhamasisha kampeni ya chanjo hiyo, Simalenga alisisitiza kuwa serikali haitavumilia vitendo vinavyohatarisha maisha ya watoto. Alieleza kuwa baadhi ya waumini wa kanisa hilo wamekuwa wakipinga chanjo kwa misingi ya imani, jambo alilosema ni kinyume cha sheria na hatari kwa jamii.


Serikali ina wajibu wa kulinda maisha ya wananchi wake. Hatuwezi kuruhusu watoto wakose chanjo kwa sababu ya imani zisizozingatia usalama wa afya,” alisisitiza.


Aliongeza kuwa tukio la kusikitisha lilitokea miaka iliyopita ambapo watoto wawili walipoteza maisha baada ya kuzuiwa kupata chanjo. Hali hiyo imeifanya serikali kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha ya wananchi.



Kwa upande mwingine, mchungaji Mathayo Samweli Nkinda kutoka kijiji cha Nyamswa alifafanua kuwa ndani ya kanisa hilo kuna makundi mawili yenye mitazamo tofauti. Alisema kundi moja linapinga chanjo, huku lingine likikubali huduma za afya bila pingamizi.



Wadau mbalimbali wamejitokeza kuunga mkono juhudi za serikali. Mwalimu Daud Jackson alitoa wito kwa viongozi wa dini kushirikiana na wataalamu wa afya badala ya kuzuia huduma muhimu. Naye mwenyekiti wa wazee wa mji wa Bariadi, Lameck Mkilila, aliipongeza serikali kwa kusimamia ipasavyo usalama wa jamii.



Mganga Mkuu wa Wilaya, Pilia Zambi, alitangaza kuwa awamu ya pili ya kampeni ya chanjo ya polio itafanyika kuanzia Mei 7 hadi 10, ikilenga kuwafikia watoto zaidi ya 178,000. Huduma zitatolewa katika shule, nyumba za ibada na maeneo mbalimbali ya jamii.



Wito umetolewa kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata chanjo, kwani ni kinga muhimu dhidi ya ugonjwa wa polio na ni hatua ya kulinda vizazi vya sasa na vijavyo.

Mwisho. 



Post a Comment

0 Comments