Na marykitoto.
Wananchi wa Kata ya Masewa katika vijiji vya Senta na Nyamikoma, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, mei 29, 2026 wamepatiwa elimu ya uhifadhi wa wanyamapori na namna ya kukabiliana na changamoto za migogoro kati ya binadamu na wanyamapori katika mkutano wa hadhara ulioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga.
Elimu hiyo ilitolewa na Muhifadhi wa Wanyamapori kutoka Pori la Akiba la Kigereshi, Floravicky Kalambo, pamoja na Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti – Kanda ya Magharibi, David G. Sulle, kwa lengo la kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori na namna ya kuishi kwa usalama katika maeneo yanayopakana na hifadhi.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Bariadi, Kwembea Seso, alisema serikali inaendelea kuimarisha juhudi za kudhibiti migogoro kati ya binadamu na wanyamapori kwa kupeleka vifaa mbalimbali vya kukabiliana na tembo waharibifu.
Alisema vifaa hivyo vinajumuisha magari, tochi maalumu pamoja na mabomu ya kufukuza wanyamapori, ambavyo vitasaidia kuongeza ufanisi katika operesheni za kuwalinda wananchi na mali zao dhidi ya uvamizi wa tembo.
Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi Daraja la Kwanza kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti – Kanda ya Magharibi, David G. Sulle, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka za uhifadhi kwa kutoa taarifa kwa wakati pindi wanapoona fisi au wanyamapori wengine wakali katika maeneo yao.
Afisa Uhifadhi Daraja Kwanza David G. Sulle kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti - Kanda ya MagharibiAlisema ushirikiano huo utasaidia kurahisisha operesheni za kudhibiti wanyama hao na kuondoa kero inayowakabili wananchi katika baadhi ya maeneo ya kata hizo.
Naye Muhifadhi wa Wanyamapori kutoka Pori la Akiba la Kigereshi, Floravicky Kalambo, alitoa elimu kuhusu changamoto za tembo, simba na fisi, huku akisisitiza kuwa si vyema wananchi kujenga makazi karibu na maeneo ya hifadhi kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza.
Muhifadhi wa Wanyamapori kutoka Pori la Akiba la Kigereshi, Floravicky KalamboKalambo alieleza kuwa wananchi wanapaswa kuzingatia sheria na miongozo ya matumizi ya ardhi, ikiwemo eneo kinga la mita 500 kutoka kwenye mipaka ya hifadhi. Alifafanua kuwa katika baadhi ya mazingira kiwango cha kifuta jasho au fidia kinaweza kutofautiana kulingana na umbali wa eneo husika kutoka kwenye hifadhi.
Aidha, alitoa elimu kuhusu umiliki wa wanyamapori na viungo vyake ikiwemo ngozi, mikia na pembe, akisisitiza kuwa umiliki wa mali hizo unapaswa kufuata sheria, taratibu na vibali vinavyotolewa na mamlaka husika.
Pia aliwahimiza wananchi wanaotaka kumiliki baadhi ya wanyamapori wanaoruhusiwa kisheria kufuata taratibu rasmi ili kupata vibali na mafunzo ya namna ya kuwatunza.
Katika hatua nyingine, Kalambo alitoa onyo kwa watu wanaofuga au kutumia wanyama aina ya fisi kwa shughuli mbalimbali kinyume na sheria za uhifadhi wa wanyamapori, akibainisha kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya hivyo.
Akihitimisha mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, alitoa rai kwa wananchi wa Kata ya Masewa na Nyamikoma kuacha kujichukulia sheria mikononi kwa kuingia porini au kuwafukuza wanyamapori pindi wanapoingia katika vijiji au mashambani.
Mhe. Simalenga alisema ni hatari kwa wananchi kujaribu kuwakabili tembo, simba, fisi na wanyamapori wengine wakali bila usimamizi wa wataalamu wa uhifadhi, kwani hatua hiyo inaweza kusababisha majeraha makubwa au hata kupoteza maisha.
Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa Maafisa Wanyamapori wa Wilaya, Askari Wanyamapori, wahifadhi kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti, Pori la Akiba la Kigereshi pamoja na mamlaka nyingine za uhifadhi ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.
"Serikali imeweka wataalamu wenye mafunzo, vifaa na uzoefu wa kushughulikia changamoto hizi. Wananchi wanapaswa kuacha kuwafukuza wanyamapori wenyewe na badala yake kutoa taarifa kwa wahusika ili kuepusha madhara yanayoweza kusababisha majeraha au vifo," alisema Mhe. Simalenga.
Mkutano huo ulitoa fursa kwa wananchi kuuliza maswali mbalimbali kuhusu changamoto za wanyamapori katika maeneo yao na kupata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa uhifadhi, huku serikali ikiahidi kuendelea kushirikiana na jamii katika kutafuta suluhisho la kudumu la migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Elimu hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori huku ikihakikisha usalama wa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopakana na hifadhi mbalimbali nchini.
Mwisho.
Na mpiga picha wetu khan kilunga.
0 Comments