Mkuu wa wilaya ya bariadi mhe.simon Simalenga akizungumza.
Na marykitoto
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Simon Simalenga, ameahidi kutoa mifuko 200 ya saruji kwa ajili ya kuunga mkono shughuli mbalimbali za maendeleo katika vijiji vya Mwantimba, Senta, Igabanilo na Nyamikoma. Msaada huo unalenga kusaidia wananchi katika ujenzi wa vyumba vya madarasa pamoja na zahanati ili kuboresha huduma za elimu na afya katika maeneo hayo.
Simalenga alitoa ahadi hiyo alipokuwa akizungumza katika mikutano mbalimbali ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kata na vijiji vya wilaya hiyo. Alisema ameridhishwa na jitihada za wananchi za kujitolea nguvu kazi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akiitaka Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi kuhakikisha inatoa ushirikiano unaohitajika ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.
Akizungumza katika Kijiji cha Mwantimba, Kata ya Masewa, Simalenga alisema ujenzi wa zahanati unaofanywa na wananchi utasaidia kupunguza changamoto ya umbali mrefu unaowakabili akina mama na wakazi wengine wanapohitaji huduma za afya.
“Hapa Mwantimba mna mpango wa kujenga zahanati ili kuwapunguzia akina mama umbali wa kwenda kujifungua na kupata huduma za afya. Mimi naahidi kuchangia mifuko 50 ya saruji kuwaunga mkono. Hapa Kijiji cha Senta mmejenga madarasa manne, nami nitawaunga mkono kwa mifuko 50 ya saruji. Igabanilo pia nitatoa mifuko 50, na Nyamikoma nitawapa mifuko 50 kwa ajili ya ujenzi wa shule. Halmashauri tuonyeshe kuwaunga mkono,” alisema Simalenga.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa maelekezo kwa vituo vya kutolea huduma za afya wilayani humo kuhakikisha wazee, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanapatiwa matibabu bure kwa mujibu wa miongozo ya serikali.
Alisisitiza kuwa makundi hayo ni miongoni mwa yanayostahili kupata huduma za afya bila malipo, hivyo ni muhimu kuhakikisha haki hiyo inazingatiwa katika vituo vyote vya afya.
Herbeth Temba kaimu mganga mkuu wa Wilaya
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kujiunga na mifumo ya bima ya afya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za matibabu na kupunguza gharama za matibabu kwa familia zao.
Meisho.
Picha na khan kilunga
0 Comments