Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

WATATU WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMTEKA NA KUMUUA MTOTO WA MIAKA 5 KWA SHINIKIZO LA TSH MILIONI 5.



Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu linawashikilia watu watatu kwa mahojiano kuhusiana na tuhuma za kumteka na kumuua mtoto mwenye umri wa miaka mitano baada ya kushindwa kupata fedha walizodai kutoka kwa baba mzazi wa mtoto huyo.


Watuhumiwa hao wametajwa kuwa ni Yumba Mayala, mwenye umri wa miaka 22, Zakayo Shija, miaka 28, na Seba Buchenja, miaka 30, wote wakazi wa Malampaka, Wilaya ya Maswa, Mkoa wa Simiyu.


Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu, tukio hilo lilitokea Agosti 6, 2026, katika Kijiji cha Gulung'washi, Kata ya Malampaka, Wilaya ya Maswa, ambapo mtoto Samike Mponeja Maleche, mwenye umri wa miaka mitano, alitekwa akiwa anachunga mifugo.


Inadaiwa kuwa mtoto huyo alitekwa na watu watatu ambao awali hawakufahamika. Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi na msako katika maeneo mbalimbali, hatua iliyowezesha kuwakamata watuhumiwa hao watatu.
Baada ya kuhojiwa na kukusanywa kwa ushahidi mbalimbali, watuhumiwa hao wanadaiwa kueleza kuwa walimteka mtoto huyo kwa lengo la kujipatia shilingi milioni tano (TSh 5,000,000) kutoka kwa baba yake mzazi.


Hata hivyo, baada ya kufanya mawasiliano na baba wa mtoto huyo na kushindwa kupata fedha hizo, watuhumiwa wanadaiwa kumuua mtoto huyo kwa kumnyonga, kisha kutundika mwili wake juu ya mti kwa lengo la kupoteza ushahidi.


Jeshi la Polisi linadaiwa kufanikiwa kupata maelekezo kutoka kwa watuhumiwa hao na kufika katika eneo ambalo mwili wa mtoto huyo ulikuwa umefichwa.


Kwa sasa, uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kukamilishwa ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.


Polisi watoa wito kwa wananchi
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limewataka wananchi kuacha kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwa lengo la kujipatia kipato, likisisitiza kuwa njia hizo hazina faida na zinaweza kusababisha madhara makubwa kwa waathirika pamoja na wahusika wenyewe.


Polisi pia limeendelea kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapobaini vitendo au mipango inayoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali.


Watuhumiwa hao bado ni watuhumiwa na hawajathibitika kuwa na hatia hadi pale mahakama itakapothibitisha vinginevyo.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments