Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA MJI BARIADI LAPOKEA TAARIFA ZA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA HALMASHAURI ROBO YA NNE 2025/2026.


Na marykitoto. 


Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Bariadi limefanya mkutano wa kujadili na kupokea taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri kwa robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026.


Mkutano huo uliofanyika tarehe 14 Agosti 2026, umeongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Mhe. Nkenyenge Charles, na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Halmashauri, Ndg. Iddi Ndabhona, Waheshimiwa Madiwani, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, wawakilishi wa taasisi mbalimbali pamoja na timu ya wataalamu wa Halmashauri.




Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Bariadi aliipongeza timu ya wataalamu kwa juhudi zinazofanywa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani. Alisema jitihada hizo zimewezesha Halmashauri kuvuka lengo la makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2025/2026.


Mwenyekiti alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usimamizi wa mapato ili kuongeza uwezo wa Halmashauri kutekeleza miradi na huduma mbalimbali kwa wananchi.



Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, aliwataka Waheshimiwa Madiwani pamoja na Wakuu wa Idara kuweka msisitizo katika usimamizi madhubuti wa ukusanyaji wa mapato, hususan katika kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya ndani.

Naomba niwasisitize timu ya Menejimenti ya Halmashauri msimamie kwa makini ukusanyaji wa mapato ili tuendelee kushikilia rekodi ya makusanyo ya 2025/2026 ambayo yamevuka lengo. Hii itasaidia kukamilisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali zilizopangwa,” amesema Mhe. Simalenga.



Mhe. Simalenga pia amesisitiza kuwa usimamizi bora wa mapato ni msingi muhimu wa kuharakisha maendeleo ya Halmashauri na kuchangia maendeleo ya Wilaya ya Bariadi pamoja na Taifa kwa ujumla.




Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Ndg. Iddi Ndabhona, amesema amepokea maelekezo na hoja zote zilizotolewa na Baraza na kuahidi kuwa yeye pamoja na timu ya Menejimenti watayatekeleza kwa weledi na kwa kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa.



Mkutano huo ni sehemu ya utaratibu wa Halmashauri wa kufanya tathmini ya utekelezaji wa mipango na shughuli za mwaka wa fedha, pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji na utoaji wa huduma kwa wananchi wa Bariadi.

Mwisho.












Post a Comment

0 Comments