Na marykitoto.
Viongozi wa dini wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhubiri na kudumisha amani kwa waumini wao, pamoja na kuepuka kauli au vitendo vinavyoweza kuchochea uvunjifu wa amani katika jamii.
Rai hiyo imetolewa Agosti 16, 2026 na Polisi Kata ya Somanda, Mkaguzi wa Polisi Mwinjuma Omary, wakati wa uchaguzi wa viongozi wa BAKWATA, uliofanyika katika Ukumbi wa Double S, uliopo Mtaa wa Kidinda, Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu.
Mkaguzi Mwinjuma amewataka viongozi hao kutumia nafasi zao kuelimisha waumini kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani, kuheshimiana na kufuata maadili mema, akisisitiza kuwa viongozi wa dini wana nafasi kubwa katika kujenga jamii salama.
Aidha, amewahimiza viongozi wa dini kuendelea kufanya kile alichokiita “doria za kiroho” kwa waumini wao, kwa kuwafuatilia na kuwaelimisha mara kwa mara kuhusu maadili, mienendo mema na madhara ya kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Amesema ushirikiano kati ya viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi ni muhimu katika kuzuia vitendo vya uhalifu, mmomonyoko wa maadili na changamoto nyingine zinazoweza kuhatarisha amani na usalama wa jamii.
Mkaguzi huyo pia amewataka viongozi wa dini kuhakikisha nyumba za ibada zinakuwa sehemu ya kujenga umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi, badala ya kuwa chanzo cha migawanyiko.
Kwa upande mwingine, amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kuwa mfano bora kwa jamii kwa kuzingatia maadili, busara na matumizi sahihi ya nafasi zao katika kuhamasisha amani na utulivu.
Ujumbe huo unakuja wakati ambapo ushirikiano wa jamii nzima unahitajika katika kulinda amani, maadili na usalama, huku viongozi wa dini wakitakiwa kutumia ushawishi wao kuijenga jamii yenye mshikamano na kuheshimiana.
Mwisho.
0 Comments