Na marykitoto.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, ametangaza kuwa kila siku ya Jumanne itakuwa siku maalumu ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika ofisi yake iliyopo Nyaumata, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu.
Mtanda amesema hatua hiyo inalenga kuwapa wananchi fursa ya kuwasilisha changamoto zinazowakabili moja kwa moja kwa uongozi wa mkoa, kupata ufafanuzi na ufumbuzi wa kero mbalimbali, zikiwemo migogoro ya kijamii, ardhi na masuala mengine yanayohitaji maamuzi ya Serikali.
“Tumetenga kila Jumanne kuwa siku maalumu ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi ofisini kwangu, ili kila mwenye changamoto apate fursa ya kuwasilisha tatizo lake na kupata ufumbuzi. Siku nyingine za wiki nitazitumia kutembelea maeneo mbalimbali ya mkoa kufuatilia miradi ya maendeleo na kuhakikisha huduma bora zinapatikana kwa wananchi.”
Amesema utaratibu huo utasaidia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu taratibu za utatuzi wa migogoro, huku wakijifunza kutokana na changamoto zilizowahi kutatuliwa na hivyo kupunguza uwezekano wa kero zinazofanana kujirudia.
Aidha, siku hiyo maalumu itakuwa chachu ya kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi, kuongeza uwajibikaji wa viongozi na kujenga imani kwa Serikali kupitia usikilizaji na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
Mtanda amesisitiza kuwa siku nyingine za wiki atazitumia kutembelea maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo, kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Serikali na kujionea hali halisi ya utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ameeleza kuwa ziara hizo zitasaidia kubaini changamoto zilizopo katika maeneo husika na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati, ili kuharakisha maendeleo na kuboresha ustawi wa wananchi.
Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha usimamizi, uwajibikaji na ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika kutatua changamoto na kusukuma mbele maendeleo ya Mkoa wa Simiyu.
Mwisho.




0 Comments