Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

MKUKI WATAKA SHERIA MPYA YA UKATILI WA KIJINSIA, MAGEUZI YA NDOA NA MIRATHI

    

Mratibu wa Kitaifa wa WiLDAF Tanzania, Wakili Anna Kulaya akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma. Picha na Kadama Malunde
Mratibu wa Kitaifa wa WiLDAF Tanzania, Wakili Anna Kulaya akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma.
Mratibu wa Kitaifa wa WiLDAF Tanzania, Wakili Anna Kulaya akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Athuman Katimba (wa pili kushoto), akiongoza uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma. Picha na Kadama Malunde
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Athuman Katimba (wa pili kushoto), akiongoza uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Athuman Katimba akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Athuman Katimba akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Athuman Katimba akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya WiLDAF, Dkt. Monica Maghoke Muhoja akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, Novemba 25,2026 jijini Dodoma.
***

Na Kadama Malunde – Dodoma

Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (MKUKI) umeitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti za kisheria na kiutendaji kukabiliana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ukiwasilisha maeneo sita ya kipaumbele yanayopaswa kufanyiwa kazi ili kulinda haki, utu na usalama wa makundi hayo kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Maeneo hayo ni pamoja na kutokomeza mauaji ya wanawake yanayohusiana na jinsia (Femicide), kutungwa kwa sheria mahsusi na jumuishi ya kupinga ukatili wa kijinsia, kutokomeza adhabu ya viboko kwa watoto, kukamilisha marekebisho ya Sheria ya Ndoa, kufanya mageuzi ya sheria za mirathi na urithi pamoja na kuimarisha upatikanaji wa haki na huduma kwa manusura wa ukatili.

Mapendekezo hayo yametolewa na Mratibu wa Kitaifa wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo barani Afrika (WiLDAF) Tanzania, Wakili Anna Kulaya, akizungumza kwa niaba ya wanachama wa MKUKI, mtandao unaojumuisha mashirika yasiyo ya kiserikali zaidi ya 200 chini ya uratibu wa WiLDAF.

Kulaya ameyawasilisha mapendekezo hayo wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa Maadhimisho ya Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Ukatili wa Kijinsia, uliofanyika Novemba 25, 2026, jijini Dodoma, akisisitiza kuwa mafanikio ya Dira 2050 hayapaswi kupimwa kwa ukuaji wa uchumi, miundombinu na teknolojia pekee, bali pia usalama, haki na ustawi wa wananchi.

“Usawa wa kijinsia, haki na utu wa binadamu si matokeo ya maendeleo pekee; ni misingi ya kuyafikia maendeleo hayo,” amesema Kulaya.

Amesema haiwezekani kujenga taifa imara wakati wanawake hawana uhakika wa usalama wao ndani ya nyumba, watoto wanakwenda shule wakiwa na hofu ya kuumizwa na wajane wanapoteza mali baada ya kufiwa na wenza wao.

Katika eneo la kwanza, MKUKI umetaka Serikali kuweka mkakati mahsusi wa kuzuia mauaji ya wanawake yanayohusiana na jinsia, kuanzisha mfumo wa ukusanyaji wa takwimu, kuimarisha utambuzi wa viashiria vya hatari na kutoa ulinzi wa haraka kwa wanawake wanaokabiliwa na vitisho na ukatili.

Kulaya amesema mifumo ya ulinzi inapaswa kuchukua hatua mapema kabla maisha ya mwanamke hayajapotea, akisisitiza kuwa mwanamke ana haki ya kukataa na kuondoka katika mahusiano yenye ukatili bila kuhatarisha maisha yake.

“Tunataka mifumo yetu ichukue hatua wakati mwanamke bado yuko hai, si baada ya maisha yake kupotea,” amesema.

Katika eneo la pili, MKUKI umeitaka Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wizara na taasisi husika kuharakisha mchakato wa kutunga Sheria Mahsusi na Jumuishi ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia, itakayozingatia pia Sheria ya Mfano ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuhusu ukatili wa kijinsia.

Amesema sheria hiyo inapaswa kutambua aina mbalimbali za ukatili, zikiwemo kupigwa, kubakwa, udhibiti wa kiuchumi, vitisho, udhalilishaji wa kisaikolojia, ukatili wa kingono na ukatili unaowezeshwa na teknolojia.

Ameeleza kuwa sheria hiyo inapaswa kuweka mfumo madhubuti wa kuzuia ukatili, kutoa amri za ulinzi, kuhakikisha manusura wanapata huduma jumuishi na kuweka wajibu wa wazi kwa taasisi zinazohusika.

“Tunataka sheria inayofanya kazi katika maisha ya wananchi, si sheria inayobaki kwenye vitabu,” amesema.

Eneo la tatu ni kutokomeza adhabu ya viboko na kulinda utu wa watoto. Kulaya amesema watoto wanapopelekwa shuleni wanatarajiwa kupata elimu katika mazingira salama, hivyo adhabu zinazoweza kuwasababishia majeraha, hofu na maumivu zinapaswa kuangaliwa upya.

Amesema wanachama wa MKUKI wameupokea kwa matumaini uamuzi wa Mahakama Kuu wa Novemba 3, 2026, katika shauri la Samweli Maduhu Mangu dhidi ya Waziri wa Elimu na mwingine, kuhusu adhabu ya viboko shuleni.

Hata hivyo, amesema wamepokea kwa masikitiko taarifa ya nia ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo, huku akiitaka Serikali kutafakari upya hatua hiyo kwa kuzingatia maslahi bora ya mtoto.

Pia, ameitaka Serikali kufanya mapitio ya sheria, kanuni na miongozo inayoruhusu adhabu ya viboko na kuwekeza katika kuwajengea uwezo walimu, wazazi na walezi kutumia mbinu za nidhamu chanya.

“Nidhamu ni muhimu katika malezi, lakini ukatili si sharti la kujenga nidhamu,” amesema.

Katika eneo la nne, MKUKI umetaka Serikali kukamilisha marekebisho ya Sheria ya Ndoa, Sura ya 29, kwa kuweka umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 18 kwa wasichana na wavulana, bila mianya inayoruhusu ndoa za utotoni.

Kulaya amesema umaskini, mila na matarajio ya kijamii vimekuwa vikiwafanya baadhi ya wasichana kuingia katika ndoa wakiwa bado watoto, hali inayokatisha ndoto zao, kupunguza fursa za elimu na kuwaweka katika mazingira ya utegemezi na ukatili.

Ameeleza kuwa mwaka 2019, Mahakama ya Rufani katika shauri la Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Rebeca Z. Gyumi ilithibitisha uamuzi kuhusu kutokubalika kikatiba kwa masharti yanayoruhusu wasichana walio chini ya miaka 18 kuolewa.

“Mtoto wa kike ana haki ya kuwa mtoto, kupata elimu, kujenga ndoto zake na kuamua mustakabali wa maisha yake. Haki hiyo haipaswi kutegemea hali ya kiuchumi ya familia yake wala mila za jamii aliyozaliwa,” amesema.

Eneo la tano linahusu mageuzi ya sheria za mirathi na urithi ili kuondoa ubaguzi wa kijinsia unaowakabili wanawake, hususan wajane wanaopoteza mali baada ya kufiwa na wenza wao.

Kulaya amesema kuna wanawake ambao kwa miaka mingi hushirikiana na wenza wao kujenga familia na kupata mali, lakini baada ya kufiwa hujikuta wakinyang'anywa mali na kunyimwa haki ya kuendelea kuishi katika nyumba walizoshiriki kujenga.

Ameiomba Serikali kuharakisha mapitio na marekebisho ya sheria za mirathi na urithi, ikiwemo masharti ya sheria za kimila zilizotangazwa kupitia Tangazo la Serikali Na. 436 la mwaka 1963, ili kuondoa ubaguzi kwa misingi ya jinsia.

“Mwanamke hapaswi kupoteza usalama wake wa kiuchumi kwa sababu amefiwa na mwenza wake. Haki yake ya kumiliki na kurithi mali lazima ilindwe na sheria,” amesema.

Katika eneo la sita, MKUKI umetaka kuimarishwa kwa upatikanaji wa haki na huduma kwa manusura wa ukatili kwa kuhakikisha wanapata msaada bila vikwazo vya kiuchumi, kijiografia au ulemavu.

Kulaya ameitaka Serikali kuimarisha Madawati ya Jinsia na Watoto ya Jeshi la Polisi kwa kuhakikisha yana watumishi wenye ujuzi, vifaa na bajeti ya kutosha, pamoja na mazingira yanayolinda usiri na utu wa manusura.

Pia, ametaka kuongezwa kwa vituo vya huduma jumuishi (One Stop Centres) na nyumba salama katika maeneo mbalimbali nchini, huku huduma za afya, msaada wa kisheria na kisaikolojia zikipatikana kwa wakati.

Amesisitiza umuhimu wa mashauri ya ukatili kushughulikiwa kwa wakati, manusura na mashahidi kulindwa dhidi ya vitisho na Serikali kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya kuzuia na kushughulikia ukatili wa kijinsia katika ngazi zote.

“Tunapohamasisha wanawake na watoto kuvunja ukimya na kutoa taarifa za ukatili, lazima tujiulize: nini kinatokea baada ya kutoa taarifa hizo? Kumwambia manusura avunje ukimya bila kuhakikisha uwepo wa mfumo utakaomlinda na kumsaidia hakutoshi,” amesema.

Akizungumzia namna ya kuhakikisha mapendekezo hayo yanatekelezwa, Kulaya amependekeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na wizara na taasisi nyingine husika kuweka utaratibu wa pamoja na Mtandao wa MKUKI wa kufanyia kazi maeneo hayo sita.

Amesema utaratibu huo unapaswa kuwa na hatua mahsusi, muda wa utekelezaji, rasilimali na taasisi zitakazowajibika ili kuhakikisha mapendekezo hayo yanazaa matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

Ameeleza kuwa wanaharakati wako tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa ushahidi, kuchangia utaalamu na kushiriki katika michakato ya mageuzi, huku wakiendelea kufuatilia utekelezaji wa ahadi na maamuzi yatakayofanywa.

“Wanawake hawahitaji huruma badala ya haki, watoto hawahitaji ukatili ili kujengewa nidhamu, na taifa halihitaji ahadi zisizoambatana na utekelezaji,” amesema Kulaya.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Athuman Katimba, ameitaka jamii kutofumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao, kwa kutoa taarifa na kuchukua hatua zinazostahili ili kulinda wanawake na watoto.

Katimba amesema Serikali inaendelea kutekeleza programu na kampeni mbalimbali za kupambana na ukatili wa kijinsia, ikiwemo Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia na Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili (2024/25–2028/29).

Ameeleza kuwa Serikali pia imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha ulinzi wa wanawake na watoto, zikiwemo kampeni ya kitaifa ya kuwalinda watoto dhidi ya matumizi ya mtandao na uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika Jeshi la Polisi, vyuo vikuu, vyuo vya kati na maeneo ya umma.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, amesema mapambano dhidi ya ukatili yanahitaji ushiriki wa wadau mbalimbali ili kuimarisha juhudi za kuondoa vitendo hivyo katika jamii.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Khatibu Kazungu, amesema mkoa huo umeweka ajenda ya kupinga ukatili kuwa sehemu ya vipaumbele vyake kwa kushirikiana na wataalamu na wadau kutoa elimu, kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa na kuhimiza ushirikiano wa taasisi zinazohusika.

Post a Comment

0 Comments