Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

RC MTANDA: PAMBA NI UTI WA MGONGO WA SIMIYU, AIPA TACOEJ USHIRIKIANO.


MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda (wa pili kushoto) akikabidhi cheti cha Usajili kwa waandishi wa Habari za Pamba na Mazingira (TACOEJ), kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa TACOEJ, Costantine Mathias, kulia ni Mary Joseph (Mjumbe) na Sitta Tuma (wa pili kulia) ambaye ni Katibu Mtendaji

Na marykitoto.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amekabidhi rasmi cheti cha usajili wa Chama cha Waandishi wa Habari za Pamba na Mazingira Tanzania (Tanzania Cotton and Environmental Journalists – TACOEJ), kilichotolewa na Serikali, huku akiahidi ushirikiano katika kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa zao la pamba.


Mtanda amekabidhi cheti hicho leo, Novemba 3, 2026, ofisini kwake mkoani Simiyu, baada ya kutembelewa na viongozi wa chama hicho, ambapo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na waandishi wa habari katika kuimarisha sekta ya pamba.


Akizungumza na viongozi hao, Mtanda amesema yuko tayari kujifunza kwa haraka kuhusu sekta ya pamba ili kufahamu changamoto zake na kushirikiana na wadau katika kuzitafutia ufumbuzi, kwa lengo la kuongeza tija na kuinua uchumi wa wakulima.


“Pamba ni uti wa mgongo wa uchumi wa Mkoa wa Simiyu. Zao hili lina changamoto nyingi sana, hivyo mimi kama Mkuu wa Mkoa ninatakiwa kujifunza haraka ili nizifahamu changamoto za zao la pamba na namna ya kuzitatua,” amesema Mtanda.


Ameongeza kuwa Serikali na TACOEJ zinapaswa kushirikiana katika kuandaa vikao vya wadau wa pamba, ili kujadili changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kukuza uzalishaji, huku waandishi wa habari wakitumia kalamu zao kuifikishia jamii elimu na taarifa sahihi.



“Ninyi kama waandishi wa habari mnatakiwa kushirikiana na mamlaka zetu kuandaa vikao vya wadau wa zao la pamba. Kisha mtatumia kalamu zenu kufikisha ujumbe kwa umma na kutoa elimu kuhusu yale tutakayokubaliana,” amesema.


Katika hatua nyingine, Mtanda amesema Mkoa wa Simiyu una dhamira ya kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka tani 133,000 zilizopo hadi kufikia tani 200,000, akibainisha kuwa lengo hilo linahitaji juhudi za pamoja za Serikali, wakulima, wadau na waandishi wa habari.


Amesisitiza kuwa ushirikiano wa karibu na wadau wa sekta ya pamba na mazingira utasaidia kukutana mara kwa mara, kubaini changamoto na kuzitatua kwa wakati, ili kuongeza tija na kuimarisha uchumi wa mkoa.



Awali, Katibu wa TACOEJ, Sitta Tumma, amesema chama hicho kitatumia taaluma na weledi wa uandishi wa habari kuhakikisha elimu sahihi kuhusu kilimo cha pamba inawafikia wakulima, kwa lengo la kuwajengea uelewa na kuwahamasisha kuongeza uzalishaji.


Amesema TACOEJ itaendelea kuwa kiungo muhimu kati ya wakulima, wadau na Serikali katika kuhabarisha, kuelimisha na kuhamasisha maendeleo ya sekta ya pamba na uhifadhi wa mazingira.

Mwisho.





Post a Comment

0 Comments