Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YANG’ARA ALGERIA, YAPATA HADHI YA MGENI WA HESHIMA.

 ​ 

Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi akiongea na Mkurugenzi wa Mirage Landmark, Zakaria Baouia

Na Kitoto Digital 

Tanzania imepata heshima ya kuwa mgeni wa heshima katika Maonesho ya Kimataifa ya Ujenzi, Makaazi na Miradi ya Miundombinu ya Bati-Est Expo 2026, yanayofanyika jijini Constantine, nchini Algeria, kuanzia Oktoba 14 hadi 16, mwaka huu.


Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, ameiwakilisha Tanzania katika maonesho hayo ya tisa, akihudhuria sherehe za ufunguzi pamoja na Gavana wa Constantine, Kerbouch Kamel.


Akizungumza na Shirika la Habari la Algeria (APS), Balozi Matinyi amewahimiza wawekezaji na wafanyabiashara wa sekta ya ujenzi nchini Algeria kuja kuwekeza Tanzania, akieleza kuwa kuna fursa nyingi zinazotokana na miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea nchini.


"Sekta ya ujenzi nchini Tanzania inachangia takriban asilimia 13 ya pato la taifa na inakua kwa wastani wa asilimia 10 kwa mwaka," amesema Balozi Matinyi.


Ameongeza kuwa Tanzania ni eneo muhimu la uwekezaji kutokana na nafasi yake ya kijiografia inayounganisha Afrika Mashariki, Kati na Kusini, pamoja na uanachama wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).


Balozi Matinyi ametaja miradi inayotoa fursa za uwekezaji kuwa ni ujenzi na upanuzi wa bandari, viwanja vya ndege, reli ya kisasa (SGR), barabara, majengo ya makazi, hospitali, shule, hoteli za kitalii na miradi ya maji na umeme.


Kupitia maonesho hayo, kampuni mbalimbali za Algeria zimeonesha nia ya kuwekeza nchini Tanzania, ikiwemo kushiriki katika miradi ya ujenzi, uzalishaji wa vifaa vya ujenzi na kununua malighafi kutoka Tanzania.


Baadhi ya kampuni hizo ni ERCM Salhi, Mirage Landmark, DEI, Fhaima, ENAP, Julex Color, Semin Algerie, Atom Metal na Golden Grass.



Aidha, Oktoba 13, 2026, Balozi Matinyi alitembelea Maonesho ya Nne ya Kimataifa ya Uwekezaji na Teknolojia ya Kilimo, Agritech Expo Annaba 2026, jijini Annaba, ambako alikutana na kampuni zilizoonesha nia ya kufanya biashara na kuwekeza Tanzania katika sekta za kilimo, mifugo, mbolea na teknolojia ya maji.


Kampuni zilizojitokeza ni pamoja na New Fertilizers, Agrosafia, Biotec-in, Alviar, Giplait, Weetel Water, Treox, Aquaox na Sofood Sogood.


Maonesho ya Bati-Est Expo 2026, yaliyoratibiwa na kampuni ya Sunflower, yameshirikisha waoneshaji 167 kutoka Algeria na nchi nyingine, zikiwemo Uturuki, Ujerumani, Uingereza, Tunisia na Misri.


Wakati huohuo, maonesho ya Agritech Expo Annaba 2026, yaliyoratibiwa na kampuni ya Incop, yameshirikisha kampuni 117 kutoka ndani na nje ya Algeria.


Hatua hiyo inaendelea kuipa Tanzania fursa ya kutangaza uwekezaji wake kimataifa, kuvutia mitaji kutoka nje na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na Algeria.

Mwisho .

Post a Comment

0 Comments