Na Kitoto Digital.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Said Mtanda, amempa siku 14 mkandarasi wa kampuni ya Sheree Company Limited kuhakikisha anachukua hatua za kuharakisha ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Meatu, kufuatia mradi huo kusuasua na kushindwa kukamilika ndani ya muda uliopangwa.
Mhe. Mtanda ametoa agizo hilo wakati wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo, ambao unakadiriwa kugharimu zaidi ya Shilingi milioni 400, huku utekelezaji wake ukiwa umefikia asilimia 40 pekee licha ya muda wa mkataba kupita kwa siku 30.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mhe. Mtanda amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia ucheleweshaji wa miradi ya maendeleo unaotokana na kushindwa kwa wakandarasi kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa mikataba waliyoingia.
"Ninampa mkandarasi siku 14 kuhakikisha anatekeleza makubaliano ya mkataba na kuchukua hatua za kuharakisha ujenzi huu. Hatutaki kuona miradi ya Serikali ikisuasua wakati wananchi wanahitaji huduma bora," amesema Mtanda.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa mkandarasi kuhakikisha changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa mradi huo zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili jengo hilo likamilike na lianze kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi huo, Katibu Tawala Msaidizi wa Sehemu ya Miundombinu Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Boniface William, amesema kuwa ujenzi huo umefikia asilimia 40, huku muda wa utekelezaji wa mkataba ukiwa umepita kwa siku 30.
Mhandisi William ameeleza kuwa moja ya sababu zilizochangia kuchelewa kwa mradi huo ni mkandarasi kukabiliwa na changamoto ya fedha za kuendesha shughuli za ujenzi, licha ya Serikali kumlipa kwa mujibu wa mkataba.
Amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha kasi ya ujenzi inaongezeka na mradi huo unakamilika kwa kuzingatia matakwa ya mkataba.
Kwa upande wake, mkandarasi wa kampuni ya Sheree Company Limited ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo umeathiriwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo uhaba wa malighafi za ujenzi, hususan saruji, pamoja na ugumu wa ardhi wakati wa shughuli za uchimbaji.
Hata hivyo, changamoto hizo zimekuja wakati ambapo muda wa mkataba tayari umepita kwa siku 30, hali iliyosababisha Mkuu wa Mkoa kutoa maelekezo ya kuchukuliwa hatua za haraka ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa wakandarasi kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia mikataba, viwango vya ubora na muda uliokubaliwa, ili kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa tija na wananchi wanapata huduma zinazokusudiwa.
Hatua ya kumpa mkandarasi siku 14 inatarajiwa kuongeza uwajibikaji na kuharakisha utekelezaji wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Meatu.
Je, mkandarasi ataweza kutumia siku hizo 14 kuonyesha mabadiliko ya kasi ya ujenzi na kutekeleza maelekezo ya Serikali? Muda uliotolewa utakuwa kipimo cha hatua zitakazochukuliwa kuondoa ucheleweshaji wa mradi huo?.
Mwisho.





0 Comments