Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

AJALI YA TRENI NA BASI MWANZA: DEREVA ATOROKA, 6 WAJERUHIWA.



Na Kitoto Digital -mwanza.

 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linamsaka dereva wa basi la Kampuni ya Africa Raha aliyekimbia baada ya basi alilokuwa akiendesha kugongwa na treni katika eneo la Fela, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, na kusababisha abiria sita kujeruhiwa.


Akizungumza kuhusu ajali hiyo iliyotokea leo majira ya saa 7 mchana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amesema basi hilo lenye namba za usajili T 715 ETS, aina ya Yutong, lilikuwa na abiria 22 likitokea Stendi ya Nyegezi kuelekea mkoani Mara.


Amesema ajali hiyo imetokea katika makutano ya barabara inayotoka Usagara kuelekea Kisesa na njia ya reli, ambapo dereva wa basi hilo alishindwa kusimama na kuchukua tahadhari kabla ya kuvuka reli.



“Dereva alishindwa kusimama na kuchukua tahadhari, hivyo kupita katika njia ya reli na kugongwa katikati na treni aina ya kiberenge,” amesema Kamanda Mutafungwa.


Kutokana na ajali hiyo, basi lilisukumwa na kutupwa pembeni, huku abiria sita wakipata majeraha na kupelekwa katika Hospitali ya Kisesa kwa ajili ya matibabu.



Kwa mujibu wa Kamanda Mutafungwa, hali za majeruhi kwa ujumla si mbaya, ingawa baadhi yao walipata mshtuko mkubwa kutokana na tukio hilo. Mmoja wa majeruhi alikimbizwa katika Hospitali ya Sekou-Toure kwa matibabu zaidi.


Kamanda Mutafungwa amewataka madereva wa magari ya abiria na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia alama za usalama, hususan katika maeneo yenye makutano ya barabara na reli.


“Madereva wanapaswa kuchukua tahadhari zaidi wanapokaribia makutano ya reli na kuheshimu alama za tahadhari zilizowekwa ili kuepusha ajali zinazoweza kusababisha majeraha, vifo na uharibifu wa mali,” amesisitiza.



Amesema eneo hilo linaendelea kuwa na shughuli za ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), hivyo ni muhimu kwa watumiaji wa barabara kufuata maelekezo ya alama zilizowekwa ili kuhakikisha usalama wao.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi, amewataka madereva na watumiaji wengine wa barabara kuongeza umakini na kuzingatia alama za barabarani.





“Madereva na watumiaji wote wa barabara wanapaswa kuwa makini na kuangalia alama za barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika,” amesema Samizi.


Naye dereva wa treni hiyo ya mizigo, Twarib Hassan Mrope, amesema treni ilikuwa ikienda kwa mwendo wa polepole wakati ajali hiyo ilipotokea, huku akieleza kuwa hajui kilichotokea kwa dereva wa basi hadi kusababisha ajali hiyo.



“Wakati ajali inatokea, tulikuwa katika mwendo wa polepole, lakini sijui ni kitu gani kilitokea kwa dereva wa basi na kusababisha ajali hiyo,” amesema Mrope.


Jeshi la Polisi linaendelea na jitihada za kumtafuta dereva huyo ili hatua zaidi zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

Mwisho.

Post a Comment

0 Comments