Na Kitoto Digital.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amewataka madiwani na watumishi wa umma wilayani Busega kuzingatia maadili, nidhamu, upendo na ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Mtanda ametoa wito huo Oktoba 12, 2026, wakati akizungumza na madiwani na watumishi hao katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea halmashauri za mkoa huo.
Amesema maadili na nidhamu ni misingi muhimu katika utumishi wa umma, inayowezesha viongozi na watumishi kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, uwajibikaji na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Amesisitiza kuwa watumishi wanapaswa kutambua dhamana waliyopewa na Serikali na kuitumia kwa manufaa ya wananchi, huku wakiepuka vitendo vinavyoweza kudhoofisha ufanisi wa kazi na kupunguza imani ya wananchi kwa viongozi wao.
Aidha, Mtanda amehimiza madiwani na watumishi wa umma kujenga mahusiano mazuri kazini kwa kuheshimiana, kusikilizana na kutatua changamoto kwa njia ya maelewano.
Amesema ushirikiano kati ya madiwani na watumishi ni muhimu katika kusimamia na kutekeleza mipango ya maendeleo, akiwataka kuweka mbele maslahi ya wananchi badala ya tofauti binafsi ili kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa wakati na huduma za kijamii zinatolewa kwa ufanisi.
Mwisho.




0 Comments