Na marykitoto.
Wanachama wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), wametembelea meli ya MV New Mwanza, wakieleza umuhimu wake katika kukuza biashara, kurahisisha usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Ziara hiyo imefanyika leo, Oktoba 13, 2026, ikiongozwa na Mwenyekiti wa MISA TAN, Edwin Soko, ikiwa na lengo la kutembelea miradi ya kimkakati na kuifahamu ili kuhabarisha umma kuhusu mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO), Abdulrahman Ally, amesema MV New Mwanza ni miongoni mwa miradi yenye uwezo mkubwa wa kufungua fursa za kiuchumi kupitia usafiri wa majini.
“Meli hii ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi, kwa kuwa inarahisisha usafiri wa wafanyabiashara, kuongeza mwingiliano wa wageni kutoka nje ya nchi na kupanua fursa za kibiashara,” amesema Ally.
Amesema meli hiyo tayari imefanya safari nane, huku tathmini iliyofanyika ikibaini mahitaji ya wateja, hususan katika usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Mwanza Kusini.
Ally ameongeza kuwa TASHICO inasubiri kukamilika kwa maandalizi ya miundombinu ya bandari hiyo ili kuwezesha meli kuanza safari zake kwa ratiba rasmi na kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA TAN, Edwin Soko, amesema ziara hiyo inalenga kuwapa waandishi wa habari fursa ya kujionea miradi ya kimkakati na kuelewa mchango wake katika maendeleo ya nchi.
"Tumefanya ziara hii ili kufahamu miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini na kuwa mabalozi wazuri wa kuitangaza kupitia vyombo vya habari, kwa lengo la kuelimisha wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa,” amesema Soko.
Amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhabarisha umma kuhusu miradi ya maendeleo, fursa zinazotokana nayo na manufaa yake kwa wananchi.
Ziara hiyo inatajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari na taasisi zinazotekeleza miradi ya kimkakati, ili wananchi wapate taarifa sahihi kuhusu fursa za maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mwisho.
Picha na Kadama Malunde.








0 Comments