Na Ellukagha Kyusa.
Daraja la Magufuli la Kigongo–Busisi limetajwa kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani, kutokana na kurahisisha usafiri, usafirishaji wa bidhaa na shughuli za kibiashara.
Awali, watumiaji wa vivuko katika eneo hilo walilazimika kutumia hadi saa mbili kuvuka Ziwa Victoria, lakini kwa sasa safari hiyo huchukua takribani dakika tano kupitia daraja hilo.
Akizungumza leo, Oktoba 13, 2026, Msimamizi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), jijini Mwanza, Mhandisi William Sanga, amesema daraja hilo limekuwa kiungo muhimu katika kuimarisha shughuli za kiuchumi na kurahisisha usafiri kwa wananchi na wafanyabiashara.
Sanga ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao ni wanachama wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), waliotembelea daraja hilo kwa lengo la kujionea manufaa ya miradi ya kimkakati nchini.
Amesema daraja hilo linaunganisha maeneo ya Kigongo na Busisi, likiwa kiungo muhimu katika ushoroba wa Ziwa Victoria unaounganisha maeneo mbalimbali, kuanzia Sirari, mpakani mwa Tanzania na Kenya, hadi nchi jirani ikiwemo Uganda.
“Daraja hili ni refu zaidi Afrika Mashariki na Kati, likiwa na urefu wa kilomita tatu, ambapo upande mmoja una kilomita 1.5 na upande mwingine kilomita 1.5,” amesema Mhandisi Sanga.
Ameeleza kuwa ujenzi wa daraja hilo ulianza Februari 25, 2020, na kukamilika mwaka 2025, kabla ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha, amesema mradi huo ulitoa ajira takribani 29,000 katika kipindi cha utekelezaji wake, huku gharama za ujenzi hadi kukamilika zikifikia zaidi ya Shilingi bilioni 700.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA TAN, Edwin Soko, amesema ziara hiyo imelenga kuwawezesha waandishi wa habari kutembelea na kufahamu miradi ya kimkakati ili waweze kuhabarisha umma kuhusu mchango wake katika maendeleo ya taifa.
Soko ameishauri Serikali kuendelea kuwashirikisha waandishi wa habari katika ziara za kutembelea miradi ya maendeleo, akieleza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kuelimisha wananchi kuhusu manufaa ya miradi hiyo na fursa zinazotokana nayo.
Amesisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhabarisha umma kuhusu miradi inayotekelezwa nchini, hatua inayoweza kuongeza uelewa wa wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mwisho.
PICHA NA KADAMA MALUNDE








0 Comments