Na marykitoto.
Serikali imeendelea kuweka msukumo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia utoaji wa mikopo ya asilimia 10, ambapo vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Mji Bariadi vimekabidhiwa hundi yenye thamani ya shilingi milioni 222.
Hafla hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji Bariadi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na halmashauri. Mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew, ambaye alikabidhi hundi hiyo kwa vikundi vinavyonufaika ikiwa ni fedha za robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango wa mikopo ya asilimia 10, Kaimu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Douglas Mshana, alisema utoaji wa mikopo hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ya kuwawezesha wananchi kuinua uchumi wao kupitia shughuli za uzalishaji mali na biashara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Nkenyenge Charles, aliwataka wanufaika wote kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanazirejesha kwa wakati ili kuwezesha vikundi vingine navyo kunufaika na mpango huo.
"Mikopo hii ni fursa ya maendeleo. Tunawaomba wanufaika kuitumia ipasavyo na kuirejesha kwa wakati ili wananchi wengine pia wapate nafasi ya kunufaika," alisema Mwenyekiti wa Halmashauri, Nkenyenge Charles.
Mgeni rasmi Naibu Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini Eng.kundo mathew
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo, Mgeni Rasmi, Naibu Waziri wa Maji na Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew, aliwataka viongozi na watendaji kuhakikisha utoaji wa mikopo unasimamiwa kwa kuzingatia uwazi, usawa na uadilifu.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya kifedha na biashara kwa wanufaika pamoja na kutumia mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa mikopo ili kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa uchumi.
"Uwazi, usawa, uadilifu, mawasiliano na elimu ya kifedha ni msingi wa mafanikio ya mpango huu. Pia ni muhimu kutumia mifumo ya kielektroniki ili kuongeza ufanisi na kuwahudumia wananchi kwa wakati," alisisitiza Mhandisi Kundo Mathew.
wawakilishi wa Maafisa wa Maendeleo ya Jamii leah kombe na Shadrack Amos waliopokea maelekezo hayo waliahidi kuyasimamia kikamilifu ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa maendeleo ya wananchi.
"Baadhi ya wanufaika
Naomi Robert kutoka kikundi cha saburi kata ya Bariadi
Mariam mlyakalulu kutoka kikundi cha ushirikiano wanawake gitoya
Elizabeth Daniel kutoka kikundi cha vijana wapambanaji kata ya somanda "
waliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Halmashauri ya Mji Bariadi kwa kuwawezesha kupata mtaji wa kuendeleza shughuli zao za kiuchumi. Waliahidi kuitumia mikopo hiyo kwa ufanisi na kuirejesha kwa wakati ili iwe chachu ya maendeleo kwao na kwa vikundi vingine vitakavyofuata.
Utoaji wa mikopo ya asilimia 10 unaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi katika ngazi ya jamii.
Mwisho.
0 Comments