Na marykitoto.
Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, amehitimisha ziara yake ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi katika kata mbalimbali za jimbo hilo, Agosti 3,2026. huku suala la migogoro ya ardhi likiibuka kuwa kilio kikubwa cha wananchi.
Katika mikutano hiyo, wakazi wengi walieleza masikitiko yao kuhusu ucheleweshaji wa upimaji wa viwanja, utoaji wa hati miliki pamoja na migogoro ya umiliki wa ardhi, hali inayowalazimu baadhi yao kufungua mashauri katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Maswa kabla ya kufikisha kesi mahakamani.
Akizungumza mbele ya wananchi, Bi. Magdalena mbuga afisa ardhi mteule kutoka Halmashauri ya Mji Bariadi, alisema changamoto nyingi zinatokana na udanganyifu unaofanywa wakati wa kuwasilisha nyaraka za umiliki wa ardhi.
"Watu wengi wamekuwa wakidanganya kupitia barua za utambulisho na mikataba ya mauziano ya ardhi. Kutokana na taarifa hizo zisizo sahihi, hati huandaliwa na baadaye migogoro hujitokeza. Tunapobaini hali hiyo, tunalazimika kuelekeza wahusika kwenda mahakamani ili tupate uamuzi wa kisheria utakaotuwezesha kufuta hati na kumpatia mmiliki halali," alisema Bi. Magdalena
Kwa upande wake, Mbunge wa Bariadi Mjini, Mhandisi Kundo Mathew, aliikosoa Ofisi ya Ardhi kwa kutofanya upimaji wa maeneo ya wananchi kwa wakati, akisema hali hiyo ndiyo chanzo kikuu cha migogoro mingi ya ardhi.
"Ofisi ya Ardhi inapaswa kutoka ofisini na kwenda kuwafikia wananchi kwa kuwafanyia upimaji wa maeneo yao na kuwapatia hati miliki kwa wakati. Bila kufanya hivyo, migogoro ya ardhi haitaisha," alisema Mhandisi Kundo.
Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Ardhi na serikali za mitaa ni muhimu katika kubaini wamiliki halali wa maeneo husika.
"Tunafanya kazi kwa kutegemeana. Serikali za mitaa ndizo zenye taarifa sahihi za wananchi na zinaweza kutusaidia kubaini mmiliki halali wa ardhi kabla ya hati kutolewa," aliongeza.
Akihitimisha mjadala huo, Mhandisi Kundo alitoa wito kwa mamlaka husika kulipa uzito suala la ardhi ili kuondoa migogoro inayowaumiza wananchi na kurejesha imani yao kwa serikali.
"Suala hili liangaliwe kwa uzito mkubwa. Tuache dhana ya kuwachonganisha wananchi na serikali; lengo letu ni kuhakikisha haki inatendeka na kila mwananchi anapata huduma stahiki kwa wakati," alisisitiza.
Ziara hiyo imeacha matumaini mapya kwa wakazi wa Bariadi Mjini, wengi wakiamini kuwa utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa utasaidia kupunguza migogoro ya ardhi na kuimarisha utoaji wa huduma za ardhi kwa ufanisi zaidi.
Mwisho.
0 Comments