Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

ZIARA YA RAIS SAMIA URUSI: FURSA MPYA ZA BIASHARA NA UWEKEZAJI KATIKA SAFARI YA TANZANIA KUELEKEA UCHUMI WA DOLA TRILIONI MOJA.



Na Beda Msimbe, TBN, St Petersburg

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, leo anahitimisha ziara yake nchini Urusi kwa kushiriki katika kongamano la kibiashara linalowakutanisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania na Urusi, sambamba na St. Petersburg International Economic Forum linalofanyika mjini St. Petersburg.


Ziara hiyo imekuja katika kipindi muhimu ambapo Tanzania inaendelea kutafuta masoko mapya, teknolojia za kisasa na mitaji ya uwekezaji ili kuharakisha maendeleo ya uchumi wake. Kupitia jukwaa hilo la kimataifa, Rais Samia anatarajiwa kuinadi Tanzania kama kitovu cha uwekezaji na biashara katika Afrika Mashariki, akieleza fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, viwanda, madini, utalii, nishati na huduma.


Ushirikiano Mpya Kati ya Tanzania na Urusi

Moja ya mafanikio makubwa ya ziara hiyo ni kuimarika kwa mahusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo. Mazungumzo yaliyofanyika yameweka msingi wa kuongeza ushirikiano katika elimu, maendeleo ya rasilimali watu, sayansi, teknolojia na ubunifu.


Urusi imeendelea kuwa miongoni mwa mataifa yenye uwezo mkubwa katika nyanja za teknolojia, uchakataji wa mazao, uzalishaji wa viwandani na tafiti za kisayansi. Ushirikiano huo unaweza kuwa chachu muhimu kwa Tanzania katika juhudi zake za kuongeza thamani ya mazao, kukuza viwanda na kuimarisha ushindani wa bidhaa zake katika soko la kimataifa.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Uchumi wa Dola Trilioni Moja

Ziara ya Rais Samia imefanyika wakati Tanzania ikijiandaa kuanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo inalenga kuifanya nchi kufikia uchumi wenye thamani ya dola za Marekani trilioni moja kwa mwaka.


Lengo hilo linahitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu, teknolojia, elimu na uzalishaji wa kisasa. Hivyo, ushirikiano wa kimkakati na mataifa yenye maendeleo ya teknolojia kama Urusi unatazamwa kuwa sehemu muhimu ya safari hiyo ya kiuchumi.


Wakati juhudi za kuvutia uwekezaji zikiendelea, takwimu za uchumi zinaonesha mwenendo mzuri wa ukuaji wa Pato la Taifa. Serikali imeeleza kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 5.5 mwaka 2024.


Akizungumza bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha mapitio ya utekelezaji wa bajeti na makadirio ya mapato na matumizi ya serikali, Khamis Mussa Omar alisema ukuaji huo umechangiwa na kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi, kuimarika kwa miundombinu ya usafiri na usafirishaji pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kilimo.


Sababu nyingine zilizochangia ukuaji huo ni kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, shughuli za ujenzi katika sekta za umma na binafsi, pamoja na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati hususan katika sekta za nishati, usafirishaji na huduma za jamii.


Kwa ujumla, ziara ya Rais Samia nchini Urusi imeonesha dhamira ya Tanzania ya kuendelea kujenga ushirikiano wa kimataifa unaolenga kuongeza uwekezaji, kuhamisha teknolojia na kufungua fursa mpya za biashara.


Kadri dunia inavyozidi kuwa ya ushindani mkubwa kiuchumi, ushirikiano wa aina hii unaweza kuwa nyenzo muhimu katika kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kisasa, wenye viwanda, teknolojia na ajira nyingi zaidi kwa wananchi wake.


Ushiriki wa Rais Samia katika Jukwaa la Kimataifa la Biashara la St Petersburg unatoa fursa ya kuitangaza Tanzania kwa wawekezaji wa kimataifa na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi. Mafanikio ya ziara hiyo yanaweza kuwa hatua nyingine muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na azma ya kuijenga Tanzania yenye uchumi mkubwa na shindani duniani.






Post a Comment

0 Comments