Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

POLISI SOMANDA WAWAJENGEA WANAFUNZI UELEWA WA KUJIKINGA NA UKATILI NA UHALIFU.

 


Na Jeshi la Polisi Kata Somanda.

Katika jitihada za kuimarisha usalama wa watoto na kuwajengea uelewa kuhusu namna ya kujikinga na vitendo vya ukatili pamoja na uhalifu, Polisi wa Kata Somanda, Mkaguzi wa Polisi Mwinjuma Omary, ametoa elimu ya ulinzi na usalama kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Somanda B.



Akizungumza na wanafunzi hao, Mkaguzi Omary alieleza umuhimu wa kutambua vihatarishi mbalimbali vinavyoweza kuhatarisha usalama wao ndani na nje ya mazingira ya shule. Elimu hiyo ililenga kuwajengea uwezo watoto kutambua mapema vitendo vya ukatili na kuchukua hatua stahiki za kujilinda.



Katika mafunzo hayo, wanafunzi walifahamishwa kuhusu maana ya ukatili, aina mbalimbali za vitendo vya ukatili vinavyoweza kutokea katika jamii, pamoja na njia za kujikinga dhidi ya vitendo hivyo. Aidha, walisisitizwa umuhimu wa kutoa taarifa kwa wazazi, walimu na Jeshi la Polisi wanaposhuhudia au kukumbana na matukio ya ukatili au vitendo vingine vya kihalifu.


Mkaguzi Omary pia aliwahimiza wanafunzi kuondoa hofu wanapokutana na askari polisi, akieleza kuwa polisi ni marafiki na walinzi wa usalama wao. Aliwataka kutokuwa na wasiwasi kutoa taarifa au kuomba msaada kutoka kwa polisi wakati wowote wanapohitaji msaada au wanapobaini jambo linaloweza kuhatarisha usalama wao.


Mbali na elimu ya ulinzi na usalama, wanafunzi hao walipatiwa elimu ya usalama barabarani. Walifundishwa namna sahihi ya kutumia barabara kwa usalama, hususan kuvuka barabara kupitia vivuko maalumu vya waenda kwa miguu (zebra crossing), ili kupunguza hatari ya ajali za barabarani.


Programu hiyo ni sehemu ya juhudi za Jeshi la Polisi kuendelea kushirikiana na taasisi za elimu katika kujenga jamii yenye uelewa wa masuala ya usalama, huku ikikuza mahusiano mazuri kati ya polisi na watoto tangu wakiwa katika umri mdogo.

 Na mpiga picha wetu khan kilunga 








Post a Comment

0 Comments