KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidia wa Polisi, Edith Swebe akiongea na waandishi wa Habari.
Na marykitoto.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limefanikiwa kuwakamata watu wawili wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya kikatili ya aliyekuwa Mhandisi wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Busega, Safiel Senzota (37).
Tukio hilo lililotikisa wakazi wa Busega na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla, linadaiwa kutokea Mei 25, 2026 katika eneo la Mwanogi, ambapo marehemu aliuawa katika mazingira ya kutatanisha yaliyohusishwa na tamaa ya mali.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 4, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi Edith Swebe, alisema kuwa mara baada ya taarifa za tukio hilo kupokelewa, Jeshi la Polisi lilianzisha uchunguzi maalumu uliowezesha kufuatilia na kumkamata mtuhumiwa mmoja jijini Dar es Salaam, alikokuwa amekimbilia baada ya kutekeleza uhalifu huo.
Kwa mujibu wa Kamanda Swebe, mahojiano ya awali yalibaini mambo mazito zaidi baada ya mtuhumiwa huyo kukiri kuhusika na mauaji hayo na kueleza kuwa alitekeleza tukio hilo kwa kushirikiana na mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari Chegeni mwenye umri wa miaka 30, ambaye inadaiwa alikuwa na ukaribu mkubwa na marehemu.
“Baada ya uchunguzi kuendelea, mtuhumiwa huyo alimtaja mwenzake ambaye naye amekamatwa na sasa wote wanashikiliwa kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria,” alisema Kamanda Swebe.
Polisi wameeleza kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo, watuhumiwa waliondoka na mali mbalimbali za marehemu zikiwemo:
Kompyuta mpakato (Laptop) aina ya HP
Simu ya mkononi aina ya Samsung
Kadi ya benki ya CRDB ya marehemu
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo kikuu cha tukio hilo kinaweza kuwa tamaa ya mali, baada ya watuhumiwa kudaiwa kupata taarifa kuwa marehemu alikuwa na fedha zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya kununua gari la mradi wake wa utengenezaji wa matofali.
Taarifa za uchunguzi zinaonesha kuwa watuhumiwa waliamini marehemu alikuwa na kiasi kikubwa cha fedha, jambo lililowasukuma kupanga na kutekeleza uhalifu huo. Hata hivyo, mpango wao haukudumu kwa muda mrefu baada ya Polisi kuingia kazini na kufanikisha kukamatwa kwao.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Simiyu limetoa onyo kali kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kwa lengo la kujipatia kipato kisicho halali, likisisitiza kuwa hakuna mhalifu atakayesalimika mbele ya sheria.
“Uhalifu haulipi. Tutawatafuta na kuwakamata wahalifu popote walipo ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria,” alisisitiza Kamanda Swebe.
Wakati uchunguzi ukiendelea, wananchi wametakiwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu na watu wanaotiliwa shaka katika maeneo yao.
Mwisho.
0 Comments