Na marykitoto
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Simon Simalenga, mei 11,2026 ameendelea kusogeza huduma karibu na wananchi baada ya kufanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, ambapo ametembelea kijiji cha Salalia kilichopo kata ya Matongo pamoja na kijiji cha Chungu kata ya Gibeshi kwa lengo la kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Simalenga amezungumzia kwa kina changamoto ya ujangili na uvamizi wa tembo katika maeneo ya wananchi, akieleza kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa fensi ya umeme ikiwa ni sehemu ya kudhibiti wanyama hao kuingia kwenye makazi na mashamba ya wananchi.
Aidha, amewasisitiza wananchi kutumia kilimo cha pilipili kama njia mojawapo ya kuwafukuza tembo, akibainisha kuwa tembo huogopa harufu kali ya pilipili hivyo mbinu hiyo inaweza kusaidia kupunguza madhara yanayosababishwa na wanyama hao.
Kwa upande wa kilimo, Mkuu huyo wa Wilaya amehimiza wananchi kuendelea na kilimo cha umwagiliaji kwa zaidi ya misimu miwili au mitatu kwa mwaka ili kuendana na mabadiliko ya tabianchi na kuongeza uzalishaji wa mazao. Amesema hatua hiyo itasaidia wananchi kuwa na uhakika wa chakula na kuongeza kipato cha familia zao.
Mhe. Simalenga pia amesema kuwa bwawa la umwagiliaji la Kasoli limefikia asilimia 92 ya utekelezaji, jambo ambalo linatarajiwa kuleta mafanikio makubwa katika shughuli za kilimo mara litakapokamilika.
Sambamba na hayo, ametoa rai kwa wafugaji kuhakikisha wanaingiza mifugo shambani kwa ajili ya kuongeza rutuba ya ardhi na kuboresha uzalishaji wa mazao, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji kwa maendeleo ya wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mhifadhi Mwandamizi kutoka Pori la Akiba Maswa, Bw. Optato Mworia, amewasihi wananchi kuacha tabia ya kupokea wageni wengi wasiokuwa na utambulisho wa kueleweka, akieleza kuwa baadhi yao hujihusisha na shughuli haramu ikiwemo ujenzi wa mazizi na malubaga ndani ya maeneo ya hifadhi.
Bw. Mworia pia amewataka wananchi kuachana na vitendo vya ujangili hususan kutega wanyama kwa ajili ya kitoweo, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni kinyume cha sheria na inahatarisha uhifadhi wa rasilimali za taifa. Aidha, amewaomba wananchi kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema.
Katika mikutano hiyo, wananchi walipata nafasi ya kueleza changamoto zao ambapo waliiomba Serikali kuwapatia mikopo hususan kwa vijana ili waweze kuachana na shughuli za ujangili na badala yake wajikite katika miradi ya maendeleo itakayowawezesha kujipatia kipato halali.
Wananchi walieleza kuwa tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana limekuwa sababu inayochangia baadhi yao kuingia katika vitendo vya ujangili, hivyo wakasisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mikopo na mafunzo ya ujasiriamali yatakayosaidia kujenga maisha bora na kuongeza fursa za ajira katika maeneo yao.
Ziara hiyo imeonekana kuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za uhifadhi pamoja na wananchi katika kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali zinazowakabili huku ikitoa matumaini mapya ya maendeleo kwa wakazi wa Wilaya ya Bariadi.
Mwisho.
0 Comments