Habari za Hivi Punde

6/recent/ticker-posts

SIMIYU YAPIGA HATUA MPYA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI.

 



Na mwandishi wetu 

Mkoa wa Simiyu umeendelea kuonyesha dhamira ya dhati katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi baada ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, Prisca Kayombo kufungua rasmi kikao kazi cha utekelezaji wa Programu ya SCALE inayolenga kuboresha mazingira na kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari za tabianchi.




Kikao hicho muhimu kimewakutanisha waratibu wa programu kutoka ngazi ya Mkoa na Halmashauri, kikifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Nyaumata, wilayani Bariadi. Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Benki ya Dunia na kuratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wenye tija wa programu hiyo katika maeneo husika.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Kayombo amesisitiza umuhimu wa waratibu kutekeleza programu hiyo kwa weledi, ubunifu na uwajibikaji ili kuhakikisha malengo ya Serikali katika uhifadhi wa mazingira na mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanafikiwa kwa ufanisi.



Aidha, amewahakikishia waratibu kutoka TAMISEMI kuwa Serikali ya Mkoa wa Simiyu itaendelea kushirikiana nao kwa karibu katika hatua zote za utekelezaji wa programu hiyo ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya kwa wananchi.


Programu ya SCALE mkoani Simiyu inatekelezwa katika Halmashauri za Maswa na Meatu, huku kitaifa ikitekelezwa katika mikoa 21 na Halmashauri 54 Tanzania Bara. 


Programu hiyo inatajwa kuwa miongoni mwa mikakati muhimu ya kuzijengea jamii uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuboresha usimamizi wa mazingira kwa maendeleo endelevu.




Post a Comment

0 Comments