Na mwandishi wetu
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limetakiwa kuendelea kujenga na kuimarisha uhusiano mzuri na wananchi kama njia muhimu ya kuimarisha ulinzi na usalama, sambamba na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mkoa huo na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa Mei 9, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi (Police Family Day) ngazi ya mkoa yaliyofanyika katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mtanda alisema ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, wananchi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ni nguzo muhimu ya kudumisha amani na utulivu nchini.
Amesisitiza kuwa wananchi ni wadau wakuu katika kuhakikisha amani inadumu, huku akibainisha kuwa maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi yanatoa fursa ya pande hizo kukutana na kuimarisha mshikamano.
“Nawapongeza kwa kuendelea kuimarisha usalama wa mkoa. Bila usalama hatuwezi kuzungumzia maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Mchango wa Mkoa wa Mwanza wa shilingi trilioni 7.2 katika pato la taifa ni kielelezo cha mazingira salama yanayowawezesha wananchi kufanya shughuli za uzalishaji,” alisema Mtanda.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa Jeshi la Polisi kupitia upandishaji vyeo kwa maofisa na askari, kuongeza vitendea kazi pamoja na ujenzi wa vituo vya polisi nchini.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbrod Mutafungwa, alisema hali ya usalama mkoani humo ni shwari tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, huku wananchi wakiendelea na shughuli zao kwa amani.
DCP Mutafungwa alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa matukio ya hapa na pale ya kihalifu, Jeshi la Polisi limekuwa likiyadhibiti kwa kushirikiana na wananchi, ambapo wahalifu hukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Jeshi la Polisi limeendelea kudhibiti matukio ya unyang’anyi, ujambazi pamoja na kuimarisha usalama barabarani kwa kushirikiana na wananchi,” alisema DCP Mutafungwa.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Familia ya Polisi yameendelea kuonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya jamii na vyombo vya ulinzi katika kujenga Mwanza salama, imara na yenye maendeleo endelevu.
Mwisho
0 Comments