Na mwandishi wetu
Serikali ya Tanzania imetangaza rasmi kuanza kwa msimu wa ununuzi wa zao la pamba kwa mwaka 2026/2027 ambapo kilo moja ya pamba itanunuliwa kwa bei elekezi ya shilingi 1,240 kwa daraja A na shilingi 620 kwa daraja B.
Tangazo hilo limetolewa katika uzinduzi wa msimu wa ununuzi wa pamba uliofanyika katika kijiji cha Mwamashimba wilayani Igunga mkoani Tabora.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Sauda Mtondoo amesema serikali itaendelea kusimamia mfumo wa malipo kwa wakulima ili kuhakikisha wanapata haki yao kwa wakati.
“Msimu wa ununuzi wa pamba 2026/2027 umefunguliwa rasmi mei 10 na bei elekezi ya kununulia pamba itakuwa shilingi 1,240 kwa kilo moja ya pamba ya daraja A na shilingi 620 kwa daraja B. Naelekeza taratibu zote zizingatiwe, wakulima walipwe kwa wakati na haki itendeke kwa kila mdau,” amesema.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania, Renatus Luneja amesema wanatarajia kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mbegu za pamba katika kijiji cha Mbutu wilayani Igunga.
Kuhusu changamoto ya baadhi ya watu kuchezea mizani, amesema mizani ya mwaka huu ikifanyiwa udanganyifu itaharibika moja kwa moja ili kuzuia vitendo vya kuwaibia wakulima. Aidha amesema malipo yatafanyika kwa fedha taslimu, simu au kupitia benki.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha amesema serikali chini ya uongozi wa Samia Suluhu Hassan imeendelea kuleta mpango wa Build Better Tomorrow (BBT) kwa lengo la kuongeza maarifa na tija kwa wakulima wa pamba.
Amesema serikali imeweka bei elekezi ili kuwalinda wakulima dhidi ya unyonyaji na kuhakikisha wanapata thamani halisi ya jasho lao.
Mwisho.
0 Comments