Na mwandishi wetu .
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Chacha Maro, amefanya mkutano maalum na wananchi wa Kijiji cha Ng’hesha, wilayani Itilima, kwa lengo la kukemea na kutoa onyo kali dhidi ya vitendo vya upigaji wa ramli chonganishi vinavyofanywa na baadhi ya waganga wa tiba asili.
Katika mkutano huo, ACP Maro ameeleza kuwa vitendo vya upigaji wa ramli chonganishi mara nyingi husababisha madhara makubwa katika jamii, ikiwemo mauaji, majeruhi, na kusambaratika kwa familia kutokana na migogoro inayochochewa na imani potofu na tuhuma zisizo na uthibitisho.
Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya mtu au watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo, ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi na vinaathiri usalama wa jamii.
Katika hatua nyingine, ACP Maro ametoa wito kwa viongozi wa jadi wa ulinzi na usalama maarufu kama sungu sungu kuepuka kujihusisha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi. Amesisitiza kuwa kufanya hivyo ni uvunjifu wa sheria na kunachangia kuongeza machafuko badala ya kusaidia kudumisha amani.
Kwa upande wake, Afisa Tarafa wa Kanadi, Lameck Lupiga, amewataka wananchi wa Kijiji cha Ng’hesha kufuata taratibu rasmi za kisheria kwa kutoa taarifa kwenye vyombo husika pindi wanapokumbana na matukio ya uhalifu, badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ng’hesha, Bunga Nselema, amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu kwa wananchi wa kijiji hicho, akisema elimu hiyo itakuwa na manufaa makubwa katika kuimarisha amani, mshikamano na uelewa wa sheria miongoni mwa wananchi.
Mkutano huo umeacha ujumbe mzito kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kuepuka imani potofu, na kushirikiana na vyombo vya dola katika kudumisha usalama wa kijamii.
Mwidho.
0 Comments