Na marykitoto
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Simon Simalenga, amelipongeza Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Bariadi kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kusimamia mipango ya ukusanyaji wa mapato, ambapo hadi kufikia Mei 18, 2026 halmashauri hiyo imefanikiwa kufikia asilimia 89.6 ya malengo waliyojiwekea.
Akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya tatu, Simalenga amesema mafanikio hayo yanaonesha ushirikiano mzuri kati ya madiwani, watendaji pamoja na wananchi katika kusukuma mbele agenda ya maendeleo ya mji wa Bariadi.
Rai kwa Madiwani na Wananchi
DC Simalenga amewataka madiwani wa kata zote kuendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu, hususan katika vikao vya maendeleo vya kata, kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa taarifa sahihi kuhusu miradi yote ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuilinda na kuithamini miradi hiyo ili iweze kuwanufaisha kwa muda mrefu.
Katika hatua nyingine, Simalenga amempongeza Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mjini, Eng. Kundo, kwa jitihada zake za kusukuma maendeleo na kuhakikisha miradi mbalimbali inakamilika kwa wakati.
Halmashauri Yajivunia Kuvuka Malengo
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Idd Ndabona, amesema baraza limeridhishwa na mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ambapo hadi sasa halmashauri imefikia asilimia 89.6 ya lengo la kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.7
Ndabona amesema wana imani kubwa kuwa ifikapo Juni 30, 2026, halmashauri hiyo itakuwa imevuka asilimia 100 ya malengo waliyojiwekea kutokana na mikakati madhubuti waliyonayo.
Walimu Wapongezwa kwa Kusimamia Miradi ya Shule
Katika kikao hicho, baraza la madiwani pia limewapongeza walimu walioonesha ubunifu na ufanisi mkubwa katika kusimamia shughuli za maendeleo shuleni, hususan miradi ya chakula mashuleni.
Walimu waliopongezwa ni Jofrey Kamgisha pamoja na Judini Mlenga.
Walimu hao wameelezwa kufanikiwa kusimamia vyema upatikanaji wa chakula shuleni kupitia kilimo katika mashamba ya shule pamoja na kutoa elimu rafiki kwa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa kuchangia chakula shuleni.
Kwa mujibu wa walimu hao, mpango huo umeleta matokeo chanya ikiwemo kupungua kwa utoro wa wanafunzi pamoja na kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi shuleni.
Madiwani Waahidi Kuendeleza Maendeleo
Akizungumza kwa niaba ya madiwani wa Halmashauri ya Mji Bariadi, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Nkenyenye S. Nkenyege, amesema wamepokea maelekezo na ushauri waliotolewa na Mkuu wa Wilaya na kuahidi kuendelea kushirikiana kuhakikisha maendeleo yanaendelea kupatikana kwa wananchi wa Bariadi.
Mwisho
0 Comments